Watu wanaanza kupoteza matumaini ya maisha kutokana na vita nchini Afrika ya Kati
Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati linasema, hadi sasa
wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, kiasi cha kuwakatisha watu wengi tamaa ya maisha
kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini mwao. Wanajeshi wa vikosi vya
waasi wanaendelea kupora mali za watu hali ambayo inaendelea kuwajengea watu hofu
na mashaka.
Waasi hawa wanaorodha ya majina ya watu wanaotaka kuwashughulikia
katika operesheni maalum. Maaskofu wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia juhudi
za kuleta haki, amani, upatanisho na mshikamano wa kweli nchini humo. Maaskofu wanabainisha
kwamba, kwa takribani miaka ishirini, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wameendelea
kushuhudia machafuko ya kisiasa yaliyopelekea watu wengi kupoteza maisha na mali zao
pamoja na kukwamisha juhudi za wananchi kujikomboa kutoka katika umaskini, ujinga
na maradhi, kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya watu.
Vita
haina macho wala pazia; imepelekea nchi yao kuwa ni kati ya nchi maskini zaidi duniani,
ingawa rasilimali wanazo, lakini kwa bahati mbaya rasilimali hii ambayo ingeweza kutumika
katika mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi maadui wakuu wa kitaifa, sasa
inatumika kwa ajili ya mauaji, nyanyaso na dhuluma za kijinsia kwa wananchi wasiokuwa
na hatia.
Shirika la Kipapa linalotoa misaada kwa Makanisa Hitaji, katika
taarifa yake linaonesha kwamba, kuanzia mwaka 2002 hadi sasa kuna jumla ya miradi
240 iliyogharimiwa na Shirika hili kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi katika
Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.
Kiasi cha Euro millioni mbili zimetumika
kwa ajili kuwajengea uwezo Makleri, kugharimia shughuli za kichungaji, ujenzi wa Makanisa
na nyumba za kitawa pamoja na kuwasomesha viongozi wa Kanisa.