Wakristo wanaalikwa kutangaza, kushuhudia na kumwabudu Mwenyezi Mungu
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 14 Aprili 2013, alitembelea na kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma.
Alipowasili, alipokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali na baadaye akaelekea kwenye
kaburi la Mtakatifu Paulo, hapo alibaki kwa kitambo kidogo akisali na baadaye, alianza
maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu.
Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu
aliwashukuru wote kwa kusema kwamba, alikuwa na furaha ya pekee kabisa kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kaburi la Mtakatifu Paulo, mwalimu wa mataifa aliyetangaza
Injili ya Kristo na kuishuhudia kwa kuyamimina maisha yake na kumwabudu kwa moyo wake
wote.
Katika somo la kwanza Baba Mtakatifu anasema, Mitume waliamriwa kwa nguvu
kutofundisha kwa jina la Yesu wala kutangaza ujumbe wake, lakini Petro na mitume wengine
wakajibu kwa ushujaa wakisema, ilikuwa imewapasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mitume
wakasonga mbele kwa ari na moyo mkuu bila kuogopa madhulumu wala vitisho, wakitangaza
Injili ya Kristo.
Baba Mtakatifu anawauliza waamini nyakati hizi, Je, wako
tayari kutangaza Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha yao? Kwenye Familia
na watu wanaoambatana nao kila siku ya maisha yao? Imani inakuja kwa kusikiliza na
ina imarishwa kwa kutangazwa.
Mitume wa Yesu walitangaza Injili ya Kristo sanjari
na kujitahidi kuwa ni waaminifu kwa Kristo aliyeyagusa na hatimaye kubadili maisha
yao, akawapatia mwelekeo mpya, kiasi kwamba, wakathubutu kuyamimina maisha hayo kama
ushuhuda kwa Kristo. Mtume Petro alipewa dhamana na Kristo kuwachunga na kuwalisha
Kondoo wake, changamoto kwa viongozi wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu kuhakikisha
kwamba, wanatekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo
na Kanisa lake bila ya kujibakiza hata kidogo.
Baba Mtakatifu anasema Injili
inapaswa kutangaza na kushuhudiwa, wajibu na dhamana ya Wakristo wote. Kila mwamini
anapaswa kujiuliza moyoni mwake ni kwa jinsi gani anavyomshuhudia Kristo katika maisha
yake, kwa kutambua kwamba, ushuhuda huu unatofautiana kadiri ya: wito na mazingira,
lakini kila mmoja anapaswa kuchangia kadiri ya nafasi yake na uhalisia wa maisha yake
ya kila siku. Kwa mfano katika kujenga na kudumisha urafiki na uhusiano mwema ndani
ya familia na maeneo ya kazi.
Baba Mtakatifu anasema, kila siku kuna watakatifu
wanaotekeleza wajibu wao kimya kimya pasi na majigambo na kwamba, kila mwamini anaweza
kushiriki utakatifu. Katika ulimwengu mamboleo kuna watu ambao wanaendelea kuteseka
kama ilivyokuwa wakati wa Mitume Petro na Paulo kwa ajili ya Injili. Kuna baadhi ya
waamini wanadiriki hata kuyamimina maisha yao ili kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo
na Kanisa lake.
Kwa hakika, Injili ya Kristo inatangazwa kwa ushuhuda amini
wa maisha. Watu wanapaswa kuona na kusikia Injili inayotangazwa na Wakristo kwa njia
ya ushuhuda wa maisha yao, ili waweze kumpatia Mungu sifa na utukufu. Hii ni changamoto
ya kutangaza Injili kwa njia ya maisha; watu waone yale yanayohubiriwa yakiwa yamemwilishwa
katika matendo kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Kanisa.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema kuwa yote haya yanawezekana ikiwa kama waamini wanamfahamu vyema
Yesu Kristo na kuendelea kufuata ile njia aliyowaonesha. Kutangaza na kuishuhudia
Injili inawezekana ikiwa kama wafuasi wa Kristo watathubutu kuwa karibu naye kama
walivyofanya Mitume wake kwa njia ya majadiliano ya maisha, ili hatimaye, waweze kumwabudu
Mwanakondoo wa Mungu aliyechinjwa, anayestahili kuabudiwa na kutukuzwa. Waamini wajenge
utamaduni wa kumwendea Mwenyezi Mungu kwa kumwomba, kumtukuza, kumshukuru lakini zaidi
kwa kumwabudu.
Kuabudu anasema Baba Mtakatifu kuna maanisha kujifunza kukaa
na kujadiliana na Mwenyezi Mungu; kuonja na kutambua uwepo wake wa daima pamoja na
kumpatia kipaumbele cha kwanza. Ni mwaliko wa kumwamini kwa kutambua kwamba, ndiye
kiongozi muhimu wa maisha ya kila mwamini, kwani Yeye ni Mungu wa maisha na historia
ya binadamu.
Hii ni changamoto ya kuvua ile miungu mikubwa na midogo, ambayo
waamini wanaitumia kama kimbilio lao, ili kujipatia uhakika wa usalama wa maisha:
miungu hii inaweza kuwa uchu wa mafanikio, madaraka na kazi; hali ya kujiona ni bora
zaidi kuliko wengine, tatizo la kujiamini kupita kiasi bila kusahau dhambi za mazoea.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao ili kubainisha ile miungu
inayowanyima nafasi ya kumwabudu Mungu wa kweli na kumpatia kipaumbele cha kwanza
katika maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko alihitimisha mahubiri yake kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, kwa kuwataka waamini kumfuasa Kristo
kwa ujasiri na uaminifu, kwani amewaonesha upendeleo wa pekee kwa kuwachagua kuwa
wafuasi wake. Anawataka kumfuasa kwa maneno na ushuhuda wa uhalisia wa maisha ya kila
siku.
Mwenyezi Mungu anawachangamotisha kuvua miungu uchwara na kuanza kumwabudu
Mungu wa kweli. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa kutangaza, kushuhudia na kumwabudu.
Bikira Maria Mama wa Mungu na wa Mitume awaombee na kuwasaidia Wakristo katika hija
yao ya ufuasi wa Kristo.
Mara baada ya Maadhimisho ya Misa Takatifu, Papa
alikwenda kutoa heshima yake kwa kwa Sanamu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, ambayo
kunako tarehe 22 Aprili 1541, Mtakatifu Inyasi wa Loyola na wafuasi wake wa kwanza
waliweka nadhiri zao za daima, tukio muhimu sana katika kuanzishwa kwa Shirika la
Wayesuit.