Viongozi wa Watawa kutoka Marekani wakutana na kuzungumza na viongozi waandamizi kutoka
Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa
Viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumatatu
tarehe 14 Aprili 2013 kwa mara ya kwanza wamekutana na kuzungumza na viongozi wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka Marekani.
Askofu mkuu Gerhard Ludwig Muller,
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa amewashukuru Watawa wanawake
kutokana na mchango wao katika sekta ya elimu, afya na huduma kwa maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Askofu mkuu Muller amewataka watawa kuendelea
kuzingatia mafundisho yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican: kwa
kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa
lake; kuendelea kuwa waaminifu kwa Mafundisho ya viongozi wa Kanisa, sanjari na kushirikiana
kwa karibu zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, mintarafu sheria za Kanisa.
Askofu
mkuu Muller amewaelezea kwa muhtasari mazungumzo yake na Baba Mtakatifu Francisko
kuhusu marekebisho yanayopaswa kufanywa katika Shirikisho la Wakuu wa Mashirika. Lengo
la mkutano kati ya viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu
ya Kanisa na Viongozi wakuu wa Mashirika ya Kitawa ni kuendeleza mshikamano wa imani
na upendo wa Kikristo, ili kuendelea kulitajirisha Kanisa kwa karama zao mbali mbali
hata kwa kizazi kijacho.