2013-04-15 09:32:31

Mitume wa Yesu walitangaza kwa ari na ujasiri mkuu kuhusu ufufuko wa Kristo kwa kutambua kwamba, walikuwa wanaongozwa na Kristo pamoja na Roho Mtakatifu


Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina na mapana ujasiri uliooneshwa na Petro pamoja na mitume wengine, licha ya kukatazwa kufundisha kwa jina la Yesu, lakini bado waliendelea kutangaza Injili ya Kristo kwa ujasiri na uhodari mkubwa wakisema kwamba, Yesu ambaye walimuua na kumtundika Msalabani, ndiye aliyefufuka kutoka katika wafu na kwamba, ni Masiha kama walivyokuwa wametabiri Manabii katika Agano la Kale.

Wakuu wa Makuhani walijitahidi bila mafanikio kuhakikisha kwamba, wanafutilia mbali Jumuiya ya Wakristo wa kwanza iliyokuwa inaibuka kwa kasi ya ajabu. Mitume wakadhulumiwa lakini hawakukata tamaa, wakaendelea kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo Mfufuka ni Bwana na Mkombozi wa Ulimwengu na kwamba sasa amekaa kuume kwa Baba yake wa mbinguni. Mitume ni mashahidi wa tukio hili. Licha ya mkong'oto wa nguvu, lakini Mitume waliendelea kufurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Kristo.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 14 Aprili 2013, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anajiuliza swali la msingi, wafuasi wa kwanza wa Yesu walipata wapi nguvu za kuweza kumtolea ushuhuda?

Walipata wapi furaha na ujasiri wa kutangaza Injili ya Kristo licha ya vizingiti walivyokumbana na vyo? Mitume wa Yesu walikuwa ni watu wa kawaida kabisa, lakini katika maisha na ushuhuda wao waliweza kuujaza mji wa Yerusalemu mafundisho juu ya Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kielelezo kwamba, Yesu Kristo Mfufuka pamoja na Roho Mtakatifu walikuwa pamoja nao, kiasi cha kuwawezesha kuhibiri kwa: ari, nguvu na ushujuaa mkubwa kuhusu Ufufuko wa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hawakuwa na woga wa mtu au kitu chochote na kwamba, madhulumu kwao ilikuwa ni heshima iliyowawezesha kufuata nyayo za Yesu kwa kumtolea ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwamba, historia ya Wakristo wa Kanisa la mwanzo ni endelevu hata kwa Wakristo wanaoishi katika ulimwengu mamboleo, kwamba, wao walimfahamu na kumwamini Yesu Kristo sanjari na kuonja uwepo wake katika hija ya maisha yao na kwamba, nguvu ya Kristo Mfufuka iliwasukuma kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushirikisha tukio la Ufufuko wa Kristo. Wakristo waliweza kuvuka vikwazo na madhulumu kwa kuonesha upendo na nguvu ya ukweli.

Baba Mtakatifu anakazia kwamba, upendo wa kidugu ni ushuhuda wa dhati ambao waamini wanaweza kuutolea ili kuonesha kwamba, kweli Yesu Kristo Mfufuka anaishi ndani mwao. Aliwaalika waamini kusali na kuwaombea Wakristo wanaoendelea kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa sala na sadaka zao waweze kuonja faraja kutoka kwa Kristo Mfufuka. Bikira Maria aliombee Kanisa, ili kwa msaada wake liweze kutangaza Injili ya Kristo kwa ari kubwa na ushujaa kwamba, kweli amefufuka nao wao ni mashahidi wa tukio hili.

Mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu alikumbushia kwamba, Jumamosi, Jimboni Venezia, Kardinali Angelo Amato alimtangaza Padre Luca Passi kuwa ni Mwenyeheri. Yeye ni mwanzilishi wa Shirika la Walei wa Mtakatifu Dorothea na Mwanzilishi wa Shirika la Watawa walimu wa Mtakatifu Dorothea. Amewaalika waamini kumshukuru Mungu kwa ushuhuda ulioneshwa na Mwenyeheri Padre Luca Passi.

Baba Mtakatifu alikumbushia pia kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia lilikuwa linaadhimisha Siku ya 89 ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, Chuo ambacho kilianzishwa na Padre Agostino Gemelli kwa kupata msaasa kutoka kwa Wakristo na watu wenye mapenzi mema. Chuo hiki kimetoa mchango mkubwa katika kuwaunda vijana ili waweze kuwajibika na daima wakitafuta mafao ya wengi.

Anawaalika waamini kuendelea kuunga mkono juhudi hizi ili ziweze kuwajengea uwezo vijana wa kizazi kipya katika kukabiliana na changamoto za maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.