2013-04-15 12:10:58

Kuna cheche kidogo za matumaini mjini Mogadishu, lakini kwa ujumla hali bado ni tete!


Bado watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha kutoka na mabomu ya kujitoa mhanga nchini Somali, kama ilivyojitokeza Jumapili iliyopita, tarehe 14 Aprili 2013. Watu watano wamepoteza maisha na wengine wengi wamejeruhiwa vibaya kutokana na mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga.

Kutokana na machafuko ya kisiasa na ukosefu wa amani na usalama, Askofu Giorgio Bertin wa Jimbo la Djibout na Msimamizi wa kitume Jimbo la Mogadishu nchini Somalia, alilazimika kuishi nje ya Jimbo lake kwa takribani miaka sita. Anasema baada ya kurejea tena Jimboni humo kwamba, kuna dalili za matumaini ingawa hali bado si shwari sana.

Tangu aliporejea ametembelea Parokia mbali mbali Jimboni mwake na kuona kwamba, hakuna tena vituo vya ukaguzi vilivyokuwa vimeenea sehemu mbali mbali za Somalia. Watu katika taabu na mahangaiko yao, wajaribu tena kurejesha amani na utulivu ingawa itawachukua muda mrefu zaidi kuweza kupata amani ya kudumu, kikolezo kikuu cha maendeleo.

Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Somalia, Caritas Somalia, limeendelea kutekeleza utume wake kwa wananchi wa Somalia waliokuwa na shida zaidi. Limeshirikiana na wadau wengine katika kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum kwenye Kambi za wakimbizi zilizotengwa kwa ajili yao.

Vita ya muda mrefu nchini Somalia imepelekea watu wengi kukosa makazi; hali ya ukosefu wa amani na usalama wa raia umepelekea pia uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kupungua kwa kiasi kikubwa, hali ambayo inachangiwa pia na ukame wa muda mrefu.

Askofu Bertin anasema, wananchi wa Somalia wanaendelea kuteseka kutokana na machafuko ya kisiasa nchini mwao. Kwa sasa wameanzisha mradi wa kufanya ukarabati katika baadhi ya Hospitali ili kutoa huduma ya afya kama kielelezo cha mshikamano wa dhati unaotolewa na Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Somalia.

Huduma na misaada ya kibinadamu bado inakabiliwa na ugumu kutokana na ukweli kwamba, sehemu kubwa ya Somalia bado inadhibitiwa na vikosi vya wanajeshi wa Al Shabaab.

Askofu Bertin akizungumza na Shirika la Habari za Kimissionari la FIDES anabainisha kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi wa Somalia wanaoishi kwenye Kanisa kuu la Mogadishu. Kwa sasa anaangalia jinsi ambavyo anaweza kuwasaidia watu hao ili Kanisa liweze kutumika kwa mambo ya Ibada, ili taratibu watu waanze kujizoesha kurudi katika maisha yao ya kawaida.

Askofu Giorgio Bertin amejiwekea mikakati ya kutaka kukutana na kujadiliana na viongozi wa Serikali ya Somalia mustakabali wa wananchi hao na jinsi ya kuwajengea tena matumaini mapya baada ya kuishi katika hali ya wasi wasi na vitisho vya vita kwa kipindi kirefu.








All the contents on this site are copyrighted ©.