2013-04-15 11:33:18

Kikanisa kilichopo kwenye Uwanja wa Ndege ni mahali muafaka pa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa


Dhamana na utume wa washauri wa maisha ya kiroho katika viwanja vya ndege vya kiraia ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumpeleka Mwenyezi Mungu kwa wafanyakazi hawa na kuwasaidia wafanyakazi hao waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika utume wao.

Ni changamoto ya kujenga utamaduni wa kumsikiliza Mungu na kusikilizana wao kwa wao, ili kwa pamoja waweze kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akakaa kati ya watu wake.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi, wakati wa ufunguzi wa Semina ya Nane kwa ajili ya Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege vya kiraia, inayofanyika mjini Cracovia, nchini Poland. Semina imefunguliwa rasmi tarehe 15 Aprili na inatarajiwa kuhitimishwa rasmi hapo tarehe 18 Arpili 2013.

Kardinali Vegliò anabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu amezungumza naye kwa njia ya: Manabii, lakini kwa wakati huu anazungumza naye kwa njia ya Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Kumbe, kila Andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kuwaadabisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kuwaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kujitaabisha kusikiliza Neno la Mungu, ili kumpatia Kristo hifadhi katika maisha ya waamini, changamoto ya watu kulindana na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Kusikiliza kwa makini Neno la Mungu kuna wawajibisha waamini kutenda kadiri ya maagizo na utashi wa Mungu, ili kufananana na Kristo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waliyempokea.

Neno la Mungu ni amana kubwa ya imani katika maisha na utume wa Kanisa. Linapaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika matendo adili. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawasaidie waamini anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kumwilisha Imani katika matendo ya huruma, kama sehemu ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Neno la Mungu likisomwa na kutafakariwa sanjari na Mafundisho ya Kanisa linaonesha utajiri mkubwa wenye uwezo wa kufundisha na kuwapatia watu hekima, ujuzi na maarifa.

Kardinali Antonio Maria Vegliò anawaalika wafanyakazi katika sekta ya usafiri wa anga kujifunza kutoka kwa Bikira Maria katika kusikiliza Neno la Mungu kwa makini na kulihifadhi katika sakafu ya mioyo yao, ili liweze kuzaa matunda ya huduma ya upendo, kama alivyofanya Bikira Maria.

Mama Kanisa anaendelea kuchangamotishwa kutoka na kwenda pembezoni mwa Jamii ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, kwani huko ndiko ambako kuna idadi kubwa ya watu wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, ujinga, umaskini, ukanimungu na dhambi, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko.

Liturujia ni mahali muafaka ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake. Hii ni changamoto kwa washauri wa maisha ya kiroho kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kujenga utamaduni wa kuadhimisha Ibada ya Neno la Mungu katika Vikanisa vilivyoko kwenye Viwanja vya Ndege. Pale inapowezekana, Ibada ya Misa Takatifu iadhimishwe pia. Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliwahi kusema kwamba, Kikanisa kilichopo kwenye Uwanja wa Ndege ni mahali muafaka pa kuweza kuadhimsiha Mafumbo ya Kanisa.

Kardinali Antonio Maria Veglio anahitimisha hotuba yake kwa wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege kwa kuhimiza kwamba, utangazaji wa Neno la Mungu unajenga na kuimarisha umoja unaowaletea waamini furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ni furaha ambayo ni zawadi kutoka kwa Kristo mwenyewe. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuwa ni watangazaji wa Injili wanaotaka kufikisha Injili ya Kristo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.