Mheshimiwa Padre Godfrey Igwebuike Onah ateuliwa na Papa kuwa Askofu mpya wa Jimbo
Katoliki Nsukka, Nigeria
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2013 amekubali ombi la Askofu Francis Emmanuel
Ogbonna Okobo wa Jimbo la Nsukka, Nigeria kutoka madarakani. Baba Mtakatifu amemteua
Mheshimiwa Padre Godfrey Igwebuike Onah, Makamu wa Gombera, Chuo Kikuu cha Kipapa
cha Urbaniana na mshauri katika Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu kuwa Askofu mpya
wa Jimbo Katoliki la Nsukka, Nigeria.
Askofu mteule Godfrey Onah alizaliwa
tarehe 18 Agosti 1956 mjini Enugu. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, akapewa
Daraja takatifu la Upadre tarehe 28 Julai 1984 kama Padre wa Jimbo Katoliki la Enugu
na kunako mwaka 1990 lilipoanzishwa Jimbo Jipya la Nsukka, akahamia huko.
Katika
maisha na utume wake kama Padre amekuwa ni Paroko Msaidizi, Jalim, Mtafiti na Padre
mshauri wa Chama cha Kitume cha Utamaduni wa Kanisa. Amewahi kuwa mkurugenzi wa taasisi
ya tafiti na tamaduni ya Kitivo cha Falsafa, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana,
Roma.
Tangu mwaka 2003 hadi mwaka 2008 ameshiriki katika Maadhimisho ya Sinodi
za Maaskofu hapa mjini Roma. Kunako mwaka 2008 akateuliwa kuwa ni Makamu wa Gombera,
Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma.