Maaskofu wa IMBISA wataka uchaguzi huru na wa haki nchini Zimbabwe
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, limezitaka
nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, kuhakikisha
kwamba, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini Zimbabwe kwa mwaka huu, unakuwa
huru na wa haki. Ombi la IMBISA limewakilishwa hivi karibuni kwa Rais Emilio Guebuza,
Rais wa Msumbiji na Mwenyekiti wa SADC kwa sasa.
Wawakilishi wa IMBISA wanaiomba
SADC ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kukoleza majadiliano ya kisiasa na hatimaye
kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinarejeshwa:
kabla, wakati na mara baada ya uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe ili kuepuka kinzani na
migogoro ya kijamii iliyoibuka kunako mwaka 2008 na hivyo kusababisha hali ngumu ya
maisha kwa wananchi wa Zimbabwe.
Ili haki, amani, utulivu, ukweli na uwazi
viweze kutawala wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi mkuu, wajumbe wa IMBISA wanasema
kuna haja kwa vyama vya kisiasa nchini Zimbabwe hasa vile vyenye ushawishi mkubwa
kuwa na makubaliano watakayotekeleza wakati wa uchaguzi mkuu na kwamba, wasimamizi
wa uchaguzi kimataifa waruhusiwe kuangalia mwendo mzima wa uchaguzi miezi mitatu kabla.
Wanaweza pia kubaki nchini Zimbabwe walau kwa mwezi mmoja baada ya uchaguzi, ili kuwa
na uhakika wa mchakato mzima wa uchaguzi. Mara nyingi vurugu na kinzani zimekuwa zikijitokeza
mara baada ya kutangaza matokeo.
Rais Emilio Guebuza amewashukuru wajumbe wa
IMBISA na kwamba, majadiliano haya yamefanyika katika hali ya maelewano ya hali ya
juu na amewashukuru wajumbe wa IMBISA kwa kuguswa na hali ya wananchi wa Zimbabwe
wakati huu wanapojiandaa kwa uchaguzi mkuu. Maaskofu wa IMBISA wamewahakikishia wakuu
wa Nchi za SADC uwepo na mchango wao katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani
na utulivu Kusini mwa Afrika.