2013-04-13 08:31:12

Kanisa linataka kuwekeza zaidi katika majiundo ya kifamilia ili kuleta mapambazuko mapya ya kifamilia


Baraza la Kipapa la Familia limeamua kuendelea kuwekeza maradufu katika majiundo ya tunu msingi za Kifamilia, ili familie zenyewe ziweze kusimama kidete kulinda na kutetea dhamana yao katika Kanisa na Jamii kwa ujumla wake.

Kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 17 Aprili 2013 kwenye Makao Makuu ya Baraza la Kipapa la Familia kutakuwa na semina mbali mbali zitakazowashirikisha wadau katika maisha na utume wa familia. Hawa ni: wanasheria, wanasayansi ya jamii, wachumi, walimu, waganga na wanasaikolojia. Wadau hawa watajadili kwa kina na mapana kuhusu umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya familia; elimu na malezi ya watoto ndani ya familia; familia na utunzaji wa wazee pamoja na mwingiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema kwamba, familia ni kitovu cha maisha ya Kijamii, ni nguzo msingi na rasilimali inayopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya mafao na ustawi wa Jumuiya ya binadamu. Hii ndiyo changamoto ambayo iko mbele ya Kanisa na Jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba; wanasiasa na watunga sera wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa familia na mahitaji yake msingi katika medani mbali mbali za maisha, ili familia iweze kutekeleza dhamana na majukumu yake.

Askofu mkuu Paglia anabainisha kwamba, Familia ni urithi wa binadamu, lakini kwa bahati mbaya, bado ni kati ya taasisi zinazokabiliwa na kinzani na magumu mengi kutoka pande mbali mbali. Hakuna maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ikiwa kama familia haitapewa uzito unaostahili. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaendelea kutikisa misingi na tunu bora za maisha ya kifamilia.

Kila mtu analo jukumu la kulinda na kutetea misingi bora ya kifamilia kwa ajili ya mafao ya wengi. Ni matumaini ya Askofu mkuu Vincenzo Paglia kwamba, semina, makongamano na katekesi za kina kuhusu tunu msingi za maisha ya Familia yatasaidia kuleta mwamko mpya katika maisha na utume wa Familia sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.