2013-04-13 11:39:08

Jumuiya ya Kikristo iwe ni chemchemi ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika Ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya themanini na tisa ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu Italia, linawaalika vijana kuwa na ujasiri, matumaini na ukarimu kwani hizi ni tunu muhimu sana katika maisha ya ujana pamoja na kuwa makini zaidi na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Maaskofu wanabainisha kwamba, chanzo kikuu cha athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni mmong'onyoko wa wa kimaadili na utu wema na kwamba, vijana wa kizazi kipya kwa sasa wanalipa kwa gharama ya maisha yao. Kuna athari kubwa zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya kifamilia, kinzani na migawanyiko ya kijamii; ukosefu wa fursa za ajira, masomo na majiundo makini kitaaluma; yote haya yanawafanya vijana wa kizazi kipya kupoteza dira na mwelekeo wa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Maaskofu wanawataka vijana kujifunga kibwebwe, ili kukuza na kuendeleza karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwani wao wanaonesha ile kiu ya ukweli na upendo mkailifu, changamoto kwa Kanisa nchini Italia kushiriki zaidi katika majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Elimu bado linaendelea kuwa ni jibu muafaka katika kukabiliana na hali ngumu pamoja na changamoto mbali mbali za maisha, kama ilivyokuwa mara tu baada ya Vita kuu ya kwanza ya dunia, Padre Agostino Gemelli alipoamua kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki, ili kuwajengea uwezo vijana katika medani mbali mbali za maisha.

Maaskofu wanabainisha kwamba, utambulisho wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki ni nafasi makini kwa wanafunzi kukabiliana na changamoto hizi kwa imani na uwezo wao wa kufikiri na kutenda; utu na heshima ya mwanadamu pamoja na mafao ya wengi vikipewa msukumo wa pekee. Kanisa kwa upande wake, linapenda kutoa fursa kwa vijana wa kizazi kipya kukua na kukomaa katika utu, maisha ya kikristo, kitamaduni, kitaaluma pamoja na kuwa na weledi utakaowawezesha kupambana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkubwa zaidi.

Jumuiya ya Kikristo iwe ni chemchemi ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Isaidie kutoa malezi endelevu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili; kwa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwashirikisha mang'amuzi mbali mbali ya maisha na kwamba, changamoto na magumu wanayokabiliana nayo yasiwapokonye kamwe matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Wazee waendelee kuwarithisha vijana amana za imani, matumaini na mapendo; daima wakiwa na ujasiri wa kuchagua ukweli utakaowasindikiza katika maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.