2013-04-12 09:42:44

Wasi wasi na hofu inazidi kutanda Korea!


Dr. Olav Fykse Tveit, katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ameisihi Korea katika ujumla wake kuondokana na kishawishi cha kutaka kufanya mashambulizi ambayo athari zake ni kubwa na badala yake, kuanza mchakato wa majadiliano ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanaisho na umoja kati ya nchi hizi mbili.

Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anayasema hayo si tu kwa sababu Korea ni kati ya nchi wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, lakini pia Baraza hili linatarajia kufanya mkutano wake mkuu wa kumi, utakaofanyika kuanzia tarehe 10 Oktoba hadi tarehe 8 Novemba 2013, mjini Busan, Korea ya Kusini.

Licha ya vitisho vinavyoendelea kujitokeza kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, kiasi cha kutishia usalama na amani duniani, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, bado nia yao ya kuadhimisha Mkutano mkuu mjini Busan iko pale pale, kwani katika hali ya wasi wasi na hofu kuu juu ya vita inayoendelea kutanda, Korea inapaswa kusikiliza tena ujumbe wa haki na amani na hili ndilo lengo lao hasa kwa wakati huu! Kuna uwezekano kabisa wa Korea kuishi katika mazingira ya haki, amani na utulivu pasi ya kuwa na chokochoko za kivita.

Mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na mambo mengine utajadili kuhusu amani na upatanisho nchini Korea. Katika mazingira kama haya anasema, Katibu mkuu, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidiplomasia ili kupata suluhu ya mgogoro huu ambao unatishia amani na utulivu duniani.

Viongozi wanaohusika wakutane na kujadiliana kuhusu tofauti zao, ili kujenga uwezo wa kuaminiana na kushirikiana ili kuepusha maafa makubwa yanayoweza kujitokeza ikiwa kama Nchi hizi mbili zitashindwa kufikia muafaka. Dr. Olav Tveit anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Korea.







All the contents on this site are copyrighted ©.