Papa kutembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Paulo, Nje ya Kuta, Jumapili tarehe 14 Aprili 2013
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 14 Aprili 2013 kuanzia saa 11:30 jioni,
anatarajiwa kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya Kuta za Roma na baadaye,
kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Katika Maadhimisho ya Ibada hii, Baba Mtakatifu
atasaidiana na Kardinali James Michael Harvey, Kardinali Codero Lanza di Montezemolo,
Kardinali Francesco Monterisi pamoja na Abate Edmund Power, OSB.
Itakumbukwa
kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita majira ya jioni aliadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Makao Makuu
ya Jimbo kuu la Roma na kuanza utume wake rasmi kama Askofu wa Jimbo la Roma. Ibada
hii ilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika ndani na nje ya Kanisa.
Kama
inavyoonekana kuwa ni sehemu ya utaratibu wake, Baba Mtakatifu Francisko huanza kwa
kusalimiana na waamini na watu wenye mapenzi mema, ambao wamekuwa wakifurika katika
matukio kama haya tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Huu ni upepo mpya wa imani
na matumaini ndani ya Kanisa.