2013-04-12 15:21:35

Papa atembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican: anawashukuru kwa moyo na majitoleo yao makubwa!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa asubuhi tarehe 12 Aprili 2013 ametembelea Makao Makuu ya Sekretarieti ya Vatican na kupokelewa na wafanyakazi na wakuu wa idara chini ya uongozi wa Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican. Hii ni ziara ya kwanza ambayo imefanywa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amependa kwenda kuwashukuru na kuwapongeza yeye mwenyewe binafsi kwa kazi kubwa na majitoleo waliyoonesha katika wakati huu wote.

Wamefanya kazi kwa masaa mengi na kujituma, kiasi kwamba, si rahisi kuweza kulipwa kwa majitoleo yote haya, lakini Yeye binafsi anapenda kuwashukuru kwa dhati kutoka moyoni mwake, hasa wakati huu anapofunga Mwezi mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kusalimiana na kila mmoja wa wafanyakazi hao na kuzungumza naye kwa muda mfupi.

Akizungumza kwa niaba ya Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican ambayo kimsingi ndiyo wasaidizi wakuu wa Papa, Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican amebainisha kwamba, Sekretarieti kuu imegawanyika katika vitengo vikuu viwili: masuala ya jumla na kitengo cha uhusiano wa kimataifa. Hii ni Familia inayoundwa na watu wenye miito, taaluma na karama mbali mbali.

Wanamshukuru sana Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea na kuzungumza nao pamoja na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuliongoza Kanisa pamoja na changamoto mbali mbali anazoendelea kutoa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wanamwomba aendelee kuwaombea ili wao pia waweze kujitoa kwa moyo wote kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.