2013-04-12 08:57:27

Mshikamano wa upendo na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii


Mfuko wa Papa ulianzishwa na Hayati Kardinali John Krol aliyeishi kunako mwaka 1910 hadi mwaka 1996 na una Makao yake Makuu mjini Philadelphia, Pennsylvania, Marekani. Lengo lilikuwa ni kumjengea uwezo wa kiuchumi Baba Mtakatifu ili kuonesha mshikamano wa upendo na huduma kwa waamini sehemu mbali mbali za dunia.

Kila mwaka wanajinyima na sadaka hii wanaikusanya na kumpelekea Baba Mtakatifu kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa katika kupambana na umaskini wa kipato na maisha ya kiroho kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na wajumbe wa Mfuko wa Papa mjini Vatican. Wajumbe hawa walipokutana na Baba Mtakatifu wamemchangia katika kapu lake kiasi cha dolla za Kimarekani 8, 600, 000. Tangu mwaka 1990 hadi leo, jumla ya dolla za Kimarekani millioni 85 zimechangwa na wanachama wa Mfuko wa Papa.

Hayo yamebainishwa na Kardinali Donald William Wuerl, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington, DC., Marekani ambaye pia ni Rais wa Taasisi za Misaada za Kanisa Katolikinchini Marekani. Anasema, hizi ni juhudi kidogo zinazopania kwa namna ya pekee kumsaidia Baba Mtakatifu kuweza kutekeleza utume wake hasa zaidi miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mfuko wa Papa umetoa fedha kwa ajili ya kusaidia majiundo ya Makleri, Watawa na Waamini Walei.

Kardinali Donald William Wuerl anasema, wanaendelea kuifanyia kazi changamoto ya Kanisa kuwa ni maskini kwa ajii ya kuonesha mshikamano wa upendo na maskini katika mchakato wa kupambana na umaskini wa kipato na maisha ya kiroho.







All the contents on this site are copyrighted ©.