2013-04-12 07:44:38

Kanisa haliwezi kuyapatia kisogo mahangaiko na matatizo ya Jamii husika, kwani linao wajibu makini ndani ya Jamii!


Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linaendelea na mkutano wake wa arobaini na moja, uliofunguliwa mapema juma hili kwa kujikita zaidi katika mmong'onyoko wa kimaadili nchini humo na mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo.

Askofu mkuu Jan Romeo Pawloski, Balozi wa Vatican nchini Congo Brazzaville na Gabon katika hotuba yake ya ufunguzi, amewaomba Maaskofu kutekeleza wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu mintarafu mang'amuzi yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mada hii inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unaopaswa kusomwa na kumwilishwa tena katika vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa. Ni sehemu ya dhamana na utume wa Mama Kanisa kufundisha maadili na utu wema ndani ya Jamii, jambo linalopaswa kutolewa ushuhuda na waamini wenyewe kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu.

Kwa upande wake, Askofu Louis Portella Mbuyu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo, amewataka Maaskofu katika mkutano wao kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Anakumbusha kwamba, Kanisa linaendelea kufanya hija na wananchi wa Congo Brazzaville katika matumaini, furaha na mahangaiko yao ya ndani. Kutokana na mwelekeo huu, Kanisa haliwezi kamwe kugeuzia kisogo mmomonyoko wa maadili na utu wema unaoendelea kujipenyeza kwa kasi kubwa nchini humo.







All the contents on this site are copyrighted ©.