Waziri mkuu wa Msumbiji akutana na kuzungumza na Papa Francisko, mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 11 Aprili 2013 amekutana na kuzungumza na
Bwana Alberto Clementino Vaquina, Waziri mkuu wa Msumbiji ambaye baadaye pia amekutana
na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na viongozi wengine waandamizi
kutoka Vatican.
Waziri mkuu wa Msumbiji amemtakia heri na matashi mema Baba
Mtakatifu Francisko kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa. Katika mazungumzo baina
ya viongozi hawa wawili, wamegusia uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Msumbiji,
ulioimarishwa kwa namna ya pekee kwa kutiliana sahihi mkataba wa ushirikiano kati
ya nchi hizi mbili, hapo tarehe 7 Desemba 2011 na kuridhiwa baada ya mwaka mmoja.
Wamepongeza mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini Msumbiji katika
nyanja mbali mbali za maendeleo na ustawi wa wananchi. Kanisa linaendelea kuchangia
kwa namna ya pekee katika sekta ya elimu, afya na maendeleo jamii, amani na utulivu.
Mwishoni
Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake Waziri mkuu wa Msumbiji Bwana Alberto Clementino
Vaquina wamezungumzia kwa ufupi changamoto na matatizo yanayoukabili Ukanda wa Afrika
Mashariki kwa ujumla.