Watu wanaohudumiwa na Caritas Italia wanamshukuru na kumpongeza Papa Francisko
Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wanaohudumiwa kwenye vituo vya huduma vinavyoendeshwa
na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Italia, ujumbe wa shukrani kwa uwepo
wao wa karibu pamoja na kuendelea kusali kwa ajili yake.
Watambue kwamba,
kwa hakika anahitaji msaada wa sala zao katika kutekeleza utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Anawahakikishia kwamba, anawakumbuka katika sala zake na kuwatakia
kheri na fanaka katika kipindi hiki cha Pasaka. Hayo yamebainishwa na Monsinyo Enrico
Feroci, Mkurugenzi wa Caritas, Italia, alipokuwa anasoma ujumbe wa Baba Mtakatifu
Francisko kwa maskini wanaohudumiwa chakula na Caritas, Italia.
Watu hawa
wanasema wameguswa kwa namna ya pekee na maneno ya Baba Mtakatifu Francisko anayesema
kwamba, wao wanayo nafasi ya pekee kabisa katika moyo wake. Tarehe 27 Machi 2013,
Caritas, Italia ilikuwa imemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa kheri na matashi
mema pamoja na kumkaribisha miongoni mwao kama Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Watu hao wanaohudumiwa na Caritas wamejadiliana wao kwa wao kuhusu matukio
kadhaa yaliyojiri ndani ya Kanisa: kung'atuka kutoka madarakani kwa Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, Conclave na hatimaye, kuchaguliwa kwa Papa Francisko.
Monsinyo Enrico Feroci ni kati ya Mapadre waliobahatika kupata chakula cha mchana
pamoja na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi kuu baada ya maadhimisho ya Ibada ya kubariki
Mafuta Matakatifu.
Maskini wa Roma wanampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu
Francisko kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Kutokana na unyenyekevu ambao ameuonesha tangu alipochaguliwa kuliongoza
Kanisa, watu hawa wanasema, wataendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa
njia ya sala. Wanamshukuru Mungu kwa kulipatia Kanisa zawadi ya Papa Francisko.