2013-04-11 09:39:53

Waraka wa kichungaji wa Pacem in Terris, unatimiza miaka 50 tangu ulipoandikwa na Papa Yohane wa XXIII


Ilikuwa ni tarehe 11 Aprili 1963 Papa Yohane wa ishirini na tatu alipochapisha Waraka wa Kichungaji: "Pacem in Terris" yaani Amani Duniani, yapata miaka hamsini iliyopita. Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani, ameadhimisha tukio hili kwa kutoa tafakari ya kina kuhusu: historia, umuhimu na changamoto zinazoendelea kujitokeza ulimwenguni katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki Marekani, kuanzia tarehe 9 hadi 10 Aprili 2013.

Kardinali Turkson anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuchagua jina hili kwa kuzingatia mambo makuu manne: vita, amani, umaskini na utunzaji bora wa mazingira. Haya pia ndiyo mawazo makuu yaliyojitokeza yapata miaka hamsini wakati Baba Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu alipoandika Waraka wake wa kichungaji, Amani Duniani, akiwa na picha ya kinzani, migogoro na vita mara tu baada ya athari za vita kuu ya Pili ya dunia iliyoleta maafa makubwa na mwendelezo wa vita baridi kati ya Mataifa makubwa duniani.

Aliona kwamba, amani ilikuwa hatarini kutoweka na kwamba, kulikuwa kuna haja ya kujenga na kuimarisha misingi ya umoja na udugu kwa kuaminiana, sanjari na utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya mwendelezo wa kazi ya uumbaji.

Kardinali Turkson anasema kwamba, kiini cha Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu ni: maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu na kama sehemu ya kanuni msingi katika sheria na ushirikiano wa kimataifa. Huu ndio msimamo ambao Vatican imekuwa ikiupatia msukumo wa pekee katika mikutano ya kimataifa inayojadili masuala ya haki, amani na upigaji rufuku wa silaha za mahangamizi.

Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu wakati anaandika Waraka huu wa kichungaji ambao unaendelea kuwa rejea katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na usalama wa kimataifa, aliona jinsi ambavyo dunia ilikuwa imegawanyika na kutawaliwa na vita baridi iliyokuwa inaendeshwa na mataifa makubwa yaani: Marekani na Urussi kwa wakati huo. Kulikuwa na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia, jambo ambalo lilijenga hofu na mashaka makubwa miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu akasimama kidete kuwaambia wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani duniani. Wakuu hawa wakasikia ujumbe wake, amani na utulivu vikarejea tena, ingawa vita baridi iliendelea kufuka moshi chini kwa chini!

Ndiyo mchango kama huu uliotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili wakati wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kukazia: ukweli, utu na heshima ya binadamu, uhuru na mshikamano wa kimataifa. Vita baridi ikafifia mataifa yakaanza kuaminiana na kujadiliana kwa pamoja mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Peter Turkson anasema, si nyakati zote sauti ya kinabii inayotolewa na Mama Kanisa imeweza kusikilizwa kwani, wakati mwingine wameipuuza na viongozi wakawasha moto wa vita, kiasi cha kuleta maafa makubwa. Kunako mwaka 2011 wakati wa mgogoro na kinzani za vita nchini Pwani ya Pembe, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alimtuma kwenda nchini humo kupeleka ujumbe wa amani, lakini kwa bahati mbaya hakuruhusiwa kuingia nchini humo, akabaki na ameshikilia Ujumbe wa Amani kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa muda wa juma zima bila mafanikio, baadaye akarudi nao! Makubwa haya!

Malengo ya Maendeleo ya Millenia pamoja na mambo mengine yanapania kufuta umaskini duniani. Kardinali Turkson anasema kuna baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa walikuwa na mawazo potofu kwa kudhani kwamba, wanaweza kuondokana na umaskini kwa kuwafutilia mbali maskini kutoka katika uso wa dunia.

Ikumbukwe kwamba, maskini wanahitaji kuwezeshwa katika elimu ili kuondokana na ujinga, wanatakiwa kujengewa uwezo wa kiuchumi ili kupambana na hali mbaya ya maisha yao na hatimaye kujiletea maendeleo endelevu, wanapaswa kusaidiwa katika maboresho ya huduma ya afya kama njia ya kuimarisha nguvu kazi katika uzalishaji mali! Huu ndio mwelekeo sahihi wa kupambana na umaskini wa hali na kipato miongoni mwa watu maskini.

Kardinali Tukrson anafafanua kwamba, Waraka wa Kichungaji wa Amani Duniani unautajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu kuhusu amani, kuwa ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu na kwamba, amani ni jina linalomwelekea Mungu mwenyewe. Amani ni neno linalowakilisha ukamilifu na lengo la maisha ya mwanadamu, kama anavyobainisha Yesu Mwenyewe kwa njia ya maisha na utume wake.

Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki na mapendo. Amani ni sehemu ya mchakato wa kila siku ya maisha ya mwanadamu inayojikita katika utafutaji wa utaratibu wa muafaka kadiri ya mapenzi ya Mungu na kwamba, amani inapatikana ikiwa kila mtu atajitahidi kutekeleza wajibu wake, kwa kuzingatia: ukweli, upendo, upatanisho na sheria. Kushindwa kwa mchakato wa amani ni vita!

Kardinali Turkson anawataka waamini na watu wenye mapenzi mema kujitajirisha na Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusiana na amani na kwamba, Waraka wa Amani Duniani ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa kujenga na kuimarisha amani duniani, hasa wakati huu wa ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Hii ni changamoto ya kudumisha ushirikiano wa kimataifa unaooongozwa na kanuni ya auni kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wana haki na wajibu wa kujenga na kuimarisha amani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika haki msingi za binadamu na maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kama anavyosali Mtakatifu Francisko wa Assisi, kila mtu anapaswa kuwa kweli ni chombo cha amani. Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kuwalinda na kuwatetea maskini kwa kuwa kweli madaraja ya amani na wala si kinzani, migogoro na vita vinavyosababisha maafa makubwa kwa Jamii. Watu wajenge na kuimarisha utamaduni wa majadiliano unaosimikwa katika ukweli, heshima na mafao ya wengi. Viongozi wa kidini wanapaswa kuonesha utashi wa kufanya majadiliano ya kina, ili amani iweze kutawala na kudumu mioyoni mwa watu.

Kwa maneno haya, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani alikuwa anahitimisha tafakari yake kwa kukazia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Pasaka alipokuwa anatoa baraka na ujumbe kwa mji wa Roma na dunia kwa ujumla, kwa kukazia amani na kuwataka watu wote wajitahidi kuwa ni vyombo vya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Jumuiya ya Kimataifa bado inakabiliwa na roho ya ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; biashara haramu ya binadamu pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Miaka hamsini ya Waraka wa kichungaji, Pacem in Terris, Amani Duniani, iwe ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani duniani.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.