Vijana, jitahidini kutubu na kumwongokea Mungu katika ujana wenu! Wakati ni huu!
Baadhi ya vijana wenzetu wameuliza mara kadhaa iwapo tulikuwa hatuadhimishi imani
kabla mpaka Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kuchukua hatua ya kuitisha mwaka
wa imani. Kwa kweli tumekuwa tukiadhimisha imani na kuiishi tangu awali, tangu enzi
za mababu. Na pia si mara
ya kwanza kuadhimisha mwaka wa imani. Kama utakumbuka zile enzi zetu vijana za mwaka
1967. Sasa usishtuke mapema juu ya nilikuwa wapi au ulikuwa wapi mwaka huo wa sitini
na saba. Tulia usikilize ujumbe kwanza halafu baada ya kipindi ndio tuongelee siku
za kuzaliwa. Halafu ukiwa katika hali hiyo hatuwezi kuelewana. Naomba utulie kidogo
tena rafiki yangu upate ung’amuzi wa mambo. Hili ndilo hema la vijana na nafasi yako
ni hapo ulipo. Karibu sana studio za Radio Vatikani. Mwaka 1967 Baba Mtakatifu
Paulo wa sita alitiisha Mwaka wa imani. Aliuweka mwaka huo kuwa mwaka wa imani katika
kumbukumbu ya karne 19 za tendo la kuifia dini mitume Petro na Paulo. Kijana hapa
inafaa ujipime kuiona imani yako kwa kina. Je unawafahamu mitume hawa wawili, Petro
na Paulo. Na je, unafahamu historia, imani na utume wao kadiri ya maandiko matakatifu
na mafundisho ya Kanisa. Au huwa usomi hata Biblia. Lakini mi naamini kuwa huwa una
soma. Kwa ufupi tu ni kwamba mitume hawa waliacha vyote na kuamua kumfuasa Kristo
na kutenda kazi ya uenezaji Injili. Mitume hawa wameanzisha jumuiya mbalimbali za
kikristu kwa kuwafikishia watu habari njema na kuwabatiza kisha kuwaweka katika kuabudu
kwa pamoja na kupendana. Waliwakumbushia imani ya dhati mara kwa mara jumuiya walizoanzisha,
au walizokutana nazo pamoja na watu mbali mbali. Mitume hawa hawakukoma kufundisha
na kuwaimarisha wenzao katika imani kwa kuwaandikia hata kwa kuwatembelea. Zaidi sana
walikubali kwa hiari kuteseka na kufa kwa ajili ya imani yao kwa Kristu. Huu ni
mfano wa kuigwa kwako kijana. Iwapo mitume hawa katika umri wao ulivyokuwa umeenda
waliamua kuongoka na kumfuasa Kristo kwa uaminifu, iwapo wao wameipigania imani na
kuvumilia mateso mpaka kifo kwa ajili ya Kristo, kwa nini wewe kijana katika umri
wako ushindwe. Kwanza sio kawaida yetu vijana wakristu kukata tamaa. Baba Mtakatifu
Paulo wa sita aliweka mwaka 1967 kwa lengo la kukualika wewe kuwa na wongofu wa ndani.
Kuwa mtu wa toba, ujitakase na umuungame Mungu kwa uhakika na kwa uaminifu. Mazingira
tunamoishi leo ni tofauti sana na nyakati za mitume Petro na Paulo. Lakini imani tunayokiri
na kuadhimisha ni ilele, haibadiliki. Wao walibuni mbinu za kufundisha, kuiungama
na kuitetea imani hii. Kijana wa leo unao ufahamu na uwezo mkubwa unaoendana na maendeleo
makubwa ya kijamii, sayansi na teknolojia. Tafadhali sana, tumia vipaji na taaluma
ulivyonavyo ili kuishuhudia imani yako, ili kuiungama na kuiishi vema. Katika umri
ulionao, mazingira unamojikuta mara nyingi vinakupelekea kuanguka katika dhambi. Jitafakari
kwa kina na ufanye toba ya kweli ndani kabisa ya nafsi yako. thamini, heshimu na adhimisha
Sakramenti ya Upatanisho. Tubu dhambi zako sasa na kila unapoanguka dhambini. Mwaka
huu wa imani jitahidi kuungama dhambi zako walau kila wiki. Mbali ya dhambi kubwa
na za mauti kuna dhambi zinazokuandama katika udhaifu wako. Mtakatifu Yohane asema
“ukisema huna dhambi unajidanganya mwenyewe na kweli haitakuwemo ndani mwako”. Fanya
toba, ungama dhambi. Jipatanishe nafsini mwako, jipatanishe na wengine na jipatanishe
na Mungu. Uwe mtu wa kusamehe. Lakini pia chukua tahadhari ya kutokuanguka katika
dhambi tena na chukua tahadhari usijeukatendwa vibaya. Bwana asema “uwe mpole kama
njiwa lakini mwelevu kama nyoka” Jitenge mbali na dhambi: tupia jela chuki na wivu;
zipige shoti tamaa mbaya; ulevi na ulafi viunguze maji moto vizithubutu tena; weka
maututi umbeya na uongo; udokozi, dhuluma na ulaghai tupia kwenye bwawa la mamba;
weka kila aina ya uovu katika kaburi lisilo na tumaini la uzima. Jiaminishe kwa Kristu
na Kanisa lake akuongoze na kukupatia utakaso, furaha, amani na ukarimu. Tubu mtu
wangu, tubu! Jitakase uwe huru! Radio Vatican itafanya sherehe kubwa pamoja na malaika
wote wa mbinguni kila utakapokuwa unafanya ungamo la ndani na la kweli. Hii bahati
ya pekee, hili jambo ni kubwa. Usilazie damu sherehe za wongofu namna hii. Ungama
kwa dhati, badili maisha uselebuke pamoja na malaika. Na kama ukiniwahi hapa studio
baada ya kuungama, sherehe hiyo gharama kwangu. Mpaka wakati mwingine tena, ni
sauti ya kinabii, Padre Celestine Nyanda.