2013-04-11 07:58:02

Kardinali Lorenzo Antonetti amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Askofu Franco Giulio Brambilla wa Jimbo kuu la Novara, Italia kufuatia kifo cha Kardinali Lorenzo Antonetti, aliyefariki dunia tarehe 10 Aprili 2013, akiwa na umri wa miaka 90. Enzi ya uhai wake aliwahi kuwa Rais msimamizi wa rasilimali ya Vatican na mwakilishi wa Kipapa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Baba Mtakatifu anaungana na Jumuiya ya Waamini wa Jimbo Katoliki la Novara, ndugu, Jamaa na wote walioguswa kwa msiba huu mzito. Anasema, ni kiongozi aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa. Katika maisha yake, akakabidhiwa nyadhifa mbali mbali, kama Balozi wa Vatican katika nchi mbali mbali duniani, Katibu mkuu wa Vatican.

Wakati wote huu ametoa ushuhuda unaomwonesha kuwa kweli ni Padre mchapakazi na mwaminifu kwa Injili. Baba Mtakatifu Francisko anachukua fursa hii kumwombea Marehemu Kardinali Lorenzo Antonetti, pumziko la milele miongoni mwa wateule wake. Anawapatia baraka zake za kitume wote wanaoomboleza msiba huu mzito.

Kardinali Lorenzo Antonetti alizaliwa tarehe 31 Julai 1922. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 26 Mei 1945. Baada ya kuhudumia Parokiani kwa takribani miaka minne, aliendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Tomaso wa Akwino na kujipatia shahada ya uzamivu katika sheria za Kanisa. Kunako mwaka 1949 hadi mwaka 1950 alijiunga na Chuo cha Kipapa cha Diplomasia.

Kunako mwaka 1951 alianza utume wake wa kidplomasia mjini Vatican: Akatumwa kufanya kazi Lebanon, Venezuela, baadaye akarudishwa mjini Vatican kuwa mkuu wa kitengo cha uhusiano wa kimataifa. 1963 hadi mwaka 1967 alikuwa mshauri kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Ufaransa na mwaka 1968 akahamishiwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Marekani.

Baba Mtakatifu Paulo wa sita, tarehe 23 Februari 1968 akamteuwa Padre Lorenzo Antonetti kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Nicaragua, utume ambao aliutekeleza hadi mwishoni mwa mwaka 1973. Akahamishiwa Kinshasa, Zaire ya Zamani ambayo kwa sasa inajulikana kama DRC hadi mwaka 1977. Akahamishiwa mjini Vatican na kuteuliwa kuwa ni Rais msimamizi wa rasilimali ya Vatican, hapa akapangiwa majukumu mbali mbali na kunako mwaka 1983 alikuwa ni kati ya viongozi wa Kanisa waliohamasisha kwa namna ya pekee uelewa na matumizi ya Sheria Mpya za Kanisa.

Askofu mkuu Lorenzo Antonetti, tarehe 23 Septemba 1988 akateuliwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Ufaransa hadi mwaka 1995, alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais msimamizi wa rasilimali ya Vatican, utume alioutekeleza hadi kufikia tarehe 5 Novemba 1998, alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Mwakilishi wa Kipapa wa Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, hadi mwaka 2006.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, kunako tarehe 21 Februari 1998 alimteuwa kuwa Kardinali. Kwa kifo cha Kardinali Lorenzo Antonetti, Dekania ya Makardinali kwa sasa ina jumla ya Makardinali 205, kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni 113 na wale wasiokuwa na haki ya kupiga wala kupigiwa kura wamebaki 92.







All the contents on this site are copyrighted ©.