2013-04-10 08:18:04

Wakristo simameni imara katika imani!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tunaendelea kukumegea utajiri uliomo kwenye ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Kipindi cha Kwaresima 2013 sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Kutujuza zaidi ni Sr. Gisela Upendo Msuya. RealAudioMP3
    “Simameni imara katika imani” (1Kor 16:13). Hivi ndivyo Mtume Paulo anavyowaandikia waamini wa Korintho. Anawahimiza wasimame imara katika imani ili wasije wakapoteza zawadi hiyo kubwa iliyo mlango wa zawadi zote za kimungu. Kanisa la Korintho lilikuwa limeanzishwa na Mtume Paulo mnamo mwaka 51. Baada ya kupanda mbegu ya imani katika mji wa Korintho, Paulo alikaa hapo mwaka mmoja na miezi sita (Mdo 18:11) akilijenga kanisa hili kwa mafundisho yake. Korintho ya wakati huo ilikuwa tayari ni mji mkubwa, wenye watu wengi na mchanganyiko, watu waliokuwa na uwezo na hadhi tofauti.

Miaka mitano baada ya kuanzishwa kwa kanisa la Korintho, unajitokeza mpasuko mkubwa unaotishia kutokomeza imani changa ya waamini wa Korintho. Tatizo la kwanza lilikuwa ni mgawanyiko baina ya waamini walioanza kujiainisha kuwa ni wafuasi wa mtume huyu au yule (Rej. 1Kor 1:12-15). Ulianza pia kujitokeza ulegevu katika kufuata kanuni za ibada (1Kor 11:17-18); na utepetevu wa kimaadili (1Kor 1:12-15; 5:1-5; 6:12-20). Msingi wa imani ulipotikiswa, wakristo wa Korintho walifikia hatua ya baadhi yao kuanza kupinga ufufuko (1Kor 15:12). Katika hali hii ya upotofu ulioanza taratibu kuota mizizi. Mtume Paulo anasimama kidete kuwakumbusha kuwa “kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure” (1Kor 15:14). Mtume Paulo analihimiza Kanisa lirudi katika njia ya misingi ya imani aliyokuwa amewafundisha. Anawaambia Wakristo wa Korintho wakeshe na kusimama imara katika imani (Rej. 1Kor 16:13).
    Matatizo na migogoro iliyokuwa inalikabili Kanisa la Korinto ilitishia kuua imani changa ya waamini wa Korintho. “Kwa vipimo vya kibinadamu hali ya Korintho haikuwa na rutuba nzuri kwa upandaji wa imani na maadili ya kikristo, lakini kisichowezekana kwa akili ya binadamu, kiliwezekana kwa nguvu ya Mungu.” Paulo anayatafutia ufumbuzi matatizo ya jumuiya hii akijengea yote juu ya msingi wa imani.

Imani maana yake ni nini?
    Imani ni zawadi tunayopata kutoka kwa Mungu. Zawadi hii inakuwa ndilo jina la uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu katika mpango wa ukombozi. Kwake yeye aliyepokea zawadi na jina hili, imani inabeba maana yake halisi; yaani, imani, “ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr 11:1). Hii ni hali ya mwanadamu kuinua moyo na akili yake kumwelekea Mungu na ahadi zake, kwa maana sisi tunaomwamini Mungu “twaenenda kwa imani, si kwa kuona” (2Kor 5:7).
  1. Haya mambo “yatarajiwayo” na “yasiyoonekana” si nadharia isiyokuwa na msingi. Haya mambo “yatarajiwayo” na “yasiyoonekana” ni tamanio la kuishi katika muungano na Mungu, Mungu ambaye tumekwishamuona katika nafsi yake ya pili; yaani, katika Yesu Kristo. Kama Yesu mwenyewe anavyosema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yn 14:9), kwa sababu imani “ni jibu la mtu kwa Mungu ambaye anajifunua mwenyewe na kujitoa mwenyewe kwa mwanadamu.” Uhusiano huu mpya kati ya Mungu na mwanadamu ambao kwa njia ya Ubatizo, mwanadamu anafanyika kuwa mwana wa Mungu, unatuwezesha kutembea katika imani ya yale tunayoyatarajia katika ulimwengu ujao.

  2. Neno la Mungu na Sakramenti zake zinatufunulia njia za imani na zinakuwa ni hakikisho la kile tunachokiamini. Na kama anavyosema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, “Kwa kusadiki na kujikabidhi kwa Mungu, tunaitikia neno la Mungu.” Mt. Ambrose anapowafundisha Wakristo wapya waliobatizwa mabadiliko yanayoendana na Sakramenti ya ubatizo waliyoipokea anasema: “Hapo awali mliona kwa macho ya mwili, sasa mnaona kwa macho ya moyo.” Hivi ndivyo wale wote waliompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wao wanavyotakiwa kuishi na kutembea kuelekea Ufalme wa Mungu. Kuona huku kwa macho ya moyo ndiyo kuona kwa imani. Hii ndio kusema anayeamini ameamua kujikabidhi kwa Mungu na anaahidi kuishi kiaminifu kadiri ya matakwa ya Neno la Mungu na ahadi zake. Tendo hili la imani kuu ya kusadiki pasipo kuona (Rej. Yn 20:29) lina tuzo lake, kama anavyotusaidia kung’amua Mt. Agostino anaposema: “Imani ni kuamini kile usichokiona, na tuzo ya imani hii ni kuona kile ulichoamini.”

  3. Imani ndio inayotupatia hakikisho la msingi ambalo juu yake tunayasimika maisha yetu yote. Imani inakuwa ni mlango usioweza kufungwa na yeyote. Kama tunavyosoma katika waraka wa sita kati ya nyaraka saba zilizoelekezwa kwa makanisa, kanisa la Filadelfia wanaambiwa: “Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga” (Ufu 3:8). Mlango huu daima uko wazi na kwa neema ya Mungu kila mtu anaweza kuupitia, iwapo tutakuwa tayari “kurekebisha maisha yetu kuendana na ukweli wa ulimwengu mpya.”

  4. Kanisa katika Mwaka huu wa imani linatuelekeza pia kukua katika imani kwa njia ya tafakari na kujifunza kwa kina Kanuni ya Imani; yaani, imani tunayoikiri. Kwa njia ya Sakramenti; yaani, imani tunayoiadhimisha. Kwa njia ya Amri Kumi za Mungu; yaani, imani tunayoiishi. Na kwa njia ya tafakari ya Sala ya Bwana; yaani, imani tunayoisali. Hivi ndivyo mafundisho ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki yalivyopangwa na kubainisha kwa ufasaha mkubwa muhtasari wa namna mkristo anavyotakiwa kuishi.










All the contents on this site are copyrighted ©.