2013-04-10 12:28:43

Kanisa linaunga mkono tafiti makini zinazozingatia maadili, utu na zawadi ya maisha tangu mtoto anapotungwa mimba!


Kanisa Katoliki linaendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo na sayansi katika tiba ya mwanadamu kwa kuzingatia maadili, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mafano wa Mungu. Linawashukuru wadau mbali mbali wanaowezesha kufanikisha tafiti za kitaalam kwa ajili ya mafao ya binadamu.

Kanisa tangu mwaka 2011 limejiwekea utaratibu wa kutaka kuelewa, kufahamu na kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na masuala ya viini tete kama sehemu ya tiba kwa kuangalia madhara yake katika Jamii husika, ndiyo maana Kanisa linaendelea kujitaabisha kufuatilia kwa makini tafiti za kisayansi katika tiba ya mwanadamu, kwa kuzingatia: zawadi ya maisha, maadili na utu wema.

Haya ni kati ya mawazo makuu yaliyojitokeza wakati Kardinali Gianfranco Ravasi Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka katika Mfuko wa Sterm For Life Foundation, kama sehemu ya Maandalizi ya Mkutano wa kimataifa unaojadili kuhusu viinitete unaoanza mjini Vatican kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 13 Aprili 2013.

Tangu Mwaka 2011 wataalam wa masuala ya viinitete na maadili kutoka ndani ya Kanisa iliwabidi kupanua zaidi ufahamu wao kwa kuangalia juu ya: tafsiri, majiundo na usambazaji wa tafiti zinazofanywa kuhusiana na tiba ya mwanadamu, ili ziweze kueleweka na watu wa kawaida. Ni changamoto iliyotolewa na Monsinyo Tomasz Trafny, Kiongozi mwandamizi kutoka kitengo cha Baraza la Kipapa la Utamaduni, Imani na Sayansi. Tafiti hizi ziliweza kuchapwa katika kitabu na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akapata nakala moja.

Mkutano wa Kimataifa kuhusu tiba ya viinitete kwa mwaka huu unalenga zaidi kutoa upembuzi yakinifu kuhusu: ushawishi, utegemezaji na ushirikiano; ili kujenga Jamii inayosimikwa katika ushawishi wa tafiti zinazozingatia maadili na utu wema; kwa kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba, tumboni mwa mama yake.

Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuungwa mkono na wadau mbali mbali wanaopania kuendeleza tafiti za kisayansi kwa muda mrefu katika masuala ya maadili ya kibayolojia na tafiti za kitamaduni.

Yote haya wanasema wawezeshaji wa mkutano huu kwamba, yamewasaidia kujenga na kuimaarisha utamduni wa majadiliano na ushirikiano katika ngazi mbali mbali: kwa kuanzia na Maajalim waliobobea katika fani hizi, taasisi za tafiti za kisayansi pamoja na vyuo vikuu kadhaa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.