Papa atuma salam za rambi rambi kufuatia kifo cha Margaret Thatcher
Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Waziri mkuu wa Uingereza Bwana
David Cameron, kufuatia kifo cha Baroness Margaret Thatcher aliyewahi kuwa Waziri
Mkuu wa Uingereza.
Katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio
Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu anatambua fadhila za kikristo zilizojionesha
kwa namna ya pekee katika utumishi wake kwa umma pamoja na kusimama kidete kuendeleza
uhuru miongoni mwa Familia ya Kimataifa.
Baba Mtakatifu anaiombea roho ya
Marehemu Magret Thatcher huruma ya Mungu, anapenda pia kuihakikishia Familia na wananchi
wa Uingereza kwa ujumla wao kwamba, yuko pamoja nao kwa njia ya sala. Anawapatia baraka
zake za kitume wote walioguswa na msiba huu.