2013-04-09 08:56:05

Margaret Thatcher, Mwanamke wa shoka anavyokumbukwa na wengi!


Viongozi wa Makanisa nchini Uingereza wanaungana na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuomboleza kifo cha Margaret Thatcher, aliyekuwa Waziri mkuu wa Uingereza kwenye miaka ya themanini, kilichotokea tarehe 8 Aprili 2013 Jijini London. Alizaliwa kunako tarehe 13 Oktoba 1925.

Askofu mkuu Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza anasema, amepokea habari za kifo cha Margaret Thatcher kwa masikitiko makubwa, kwani ni kiongozi aliyeongoza watu wake kama Mbunge na Waziri mkuu kwa majitoleo makubwa. Kwa niaba ya Kanisa Katoliki nchini Uingereza anapenda kuchukua fursa hii kwa ajili ya kuiombea roho ya Marehemu Tthatcher ili aweze kupumzika kwa amani pamoja na kuendelea kuiombea familia yake na wote wanaomboleza kwa wakati huu.

Naye Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury, Uingereza, katika salam zake za rambi rambi anasema, Hayati Margaret Thatcher alijitoa kikamilifu kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi wake, akaungama imani yake katika matendo.

Askofu mkuu Welby anatuma salam za rambi rambi kwa watoto wa Hayati Margaret Thacther, ndugu, jamaa na marafiki wanaoomboleza kwa msiba huu mzito. Ni jambo la haki kabisa kumshukuru Hayati Margaret Thatcher kutokana na majitoleo yake makuu kwa wananchi wa Uingereza.

Margaret Thatcher amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87. Alibahatika kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa takribani miaka kumi na moja, kipindi ambacho aliweka misingi thabiti ya mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini mwake. Ni kiongozi ambaye kwa mara ya kwanza katika historia ya Uingereza aliweza kubadilisha mfumo wa uchumi kwa kukumbatia sera za soko huria, hali ambayo iliiwezesha Uingereza kucharuka katika uchumi kiasi hata cha kutunisha misuri yake dhidi ya Marekani.

Wachunguzi wa masuala ya kijamii wanasema kwamba, Hayati Thatcher ni kiongozi ambaye hakuguswa sana na kilio cha maskini, ingawa ni mtu aliyeonja athari za Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Alikuwa na falsafa iliyomwezesha kukabiliana na matatizo na changamoto uso kwa uso bila kukwepa wala kupindisha msimamo wake, pengine ni kutokana na falsafa hii hadi leo hii anakumbukwa na wengi kama "Mwanamke wa Shoka". Alijimwaga kwenye uwanja wa siasa akiwa ni msichana mbichi kabisa tangu mwaka 1950.

Kunako mwaka 1951 akafunga ndoa na Bwana Denis Tharcher na kbahatika kupata watoto wawili. Mme wake ni kati ya watu waliomsaidia sana katika masuala ya uongozi kwa kumtia shime kusonga mbele pale alipokumbana na vizingiti. Kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa Mbunge kunako mwaka 1959. Akiwa Waziri mkuu alibinafisha Mashirika na Makampuni makubwa yaliyokuwa yanamilikiwa na kuendeshwa na Serikali. Akauza na kuwamilikisha wapangaji baadhi ya nyumba za Serikali.

Kama Waziri mkuu wa Uingereza hakubadilisha msimamo wake hata mara moja kuhusu mgomo wa Umoja wa Wafanyakazi wa Migodi nchini Uingereza, mgomo ambao ulidumu kwa majuma 51 kunako mwaka 1984, wakipinga Serikali kufunga baadhi ya machimbo nchini Uingereza. Wagomaji hatimaye, walisalimu amri na kurudi kazini bila ya masharti. Kunako mwaka 1984 aliponea chupu chupu baada Kikosi cha IRA kulipua bomu lililopelekea viongozi kadhaa wa Serikali kupoteza maisha, Thatcher na Mumewe wakatoka wakiwa wazima!

Kuanzia miaka tisini, wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema kwamba, Thatcher alianza kujiamini kupita kiasi hata kushindwa kusikiliza maoni yaliyokuwa yanatolewa na Mawaziri pamoja na viongozi wengine wa Serikali. Migomo na machafuko na kinzani za kijamii zikawa ni wimbo wa kila siku nchini Uingereza, jambo lililopelekea kuachia ngazi kwa ajili ya manufaa ya umma.

Margaret Thatcher, Mwanamke wa shoka, akashuka kutoka katika Jukwaa la Kisiasa akitokwa na machozi bila kuamini kwamba, ulimwengu ni tambara bovu! Huyu ndiye ambaye viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaomboleza kutoka na kifo chake.







All the contents on this site are copyrighted ©.