Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 9 Aprili 2013 amekutana na kuzungumza na
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon alipomtembelea mjini Vatican. Mazungumzo
ya viongozi hawa wawili yamedumu kwa takribani dakika ishirini. Viongozi hawa wawili
wamejadili kuhusu: haki na amani; mafao ya wengi na haki msingi za binadamu.
Wamejadili
kwa kina pia kuhusu vita, migogoro na kinzani zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali
mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee, Barani Afrika. Biashara haramu ya binadamu,
tatizo na wakimbizi na wahamiaji ni kati ya mambo yaliyojadiliwa wakati wa mazungumzo
ya viongozi hawa wawili pamoja na kuangalia jinsi ambapo Jumuiya ya Kimataifa inaweza
kuzuia vita isitokee; umuhimu wa kujenga na kuimarisha mshikamano wa kimataifa pamoja
na kuibua mikakati ya maendeleo endelevu. Baba Mtakatifu amebainisha pia mchango wa
Kanisa katika ustawi na maendeleo ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia.
Katibu
mkuu aliambatana na ujumbe wa watu kumi na wawili waliopokelewa kwa gwaride la heshima
walipowasili mjini Vatican. Katibu mkuu amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba,
Umoja wa Mataifa na Vatican wanashirikisha malengo na mawazo kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya binadamu.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi
wa habari amebainisha kwamba, hata Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo ya Millenia unapania kupambana na baa la umaskini duniani kwa kuwajengea
watu uwezo wa kupambana na hali yao ya maisha.
Katibu mkuu amesema, wamejadili
kuhusu haki jamii na umuhimu wa kuongeza kasi ya kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia.
Amefurahishwa na azma ya Baba Mtakatifu Francisko kutaka kuwa ni daraja la Jumuiya
mbali mbali za kiimani, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na
mshikamano na uvumilivu kati ya watu.
Papa Francisko ni kiongozi wa amani
mwenye malengo thabiti na kwa hakika ni sauti ya wanyonge. Katibu mkuu anasema amemkaribisha
Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Umoja wa Mataifa atakapopata nafasi katika ratiba
zake.
Katibu mkuu amemzawadia Baba Mtakatifu Francisko kitabu ambacho kimeandikwa
katika lugha sita zinazotumiwa na Umoja wa Mataifa katika mikutano yake. Baba Mtakatifu
amempatia Katibu mkuu zawadi ya Picha ya Mji wa Roma na baadaye akawagawia Rozari
Takatifu wajumbe waliokuwa kwenye msafara wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katibu
mkuu pia amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu
mkuu wa Vatican pamoja na ujumbe wake. Kumbu kumbu zinaonesha kwamba, tangu uongozi
wa Papa Yohane wa ishirini na tatu, Makatibu wakuu wa Umoja wa Mataifa saba wamekwisha
kutembelea mjini Vatican na kuzungumza na Viongozi wa Kanisa.
Katibu mkuu
wa Umoja wa Mataifa akiwa nchini Italia, amekutana na kuzungumza na Rais Giorgio Napolitano,
Professa Mario Monti, Waziri mkuu wa Italia pamoja na Wakuu wa Bunge la Italia.