Fadhila ya unyenyekevu inajionesha kwa namna ya ajabu katika Fumbo la Pasaka
Unyenyekevu ni kanuni ya dhahabu inayomwezesha mwamini kukua na kukomaa katika fadhila
ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Ni maneno yaliyosemwa na Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa
cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 8 Aprili 2013.
Ibada hii imehudhuriwa na wafanyakazi wa Sekretarieti ya Vatican pamoja na
Masista wa Upendo waliorudia tena nadhiri zao za kitawa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko.
Anasema, historia ya maisha ya imani inafumbatwa kwa namna ya pekee katika hali ya
unyenyekevu, kama inavyojionesha katika Fumbo la Umwilisho, Yesu, Nafsi ya Pili ya
Fumbo la Utatu Mtakatifu alipoutwaa mwili na hatimaye kuzaliwa na Bikira Maria, katika
mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa Yeye hakutenda dhambi. Mwana wa Mungu
alijinyenyekesha akawa mtii hata kukubali kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani.
Huu
ndio unyenyekevu uliooneshwa na Bikira Maria, aliyekubali mpango wa Mungu katika maisha
yake, kama ilivyokuwa hata kwa Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Mtoto Yesu.
Itakumbukwa
kwamba, tarehe 8 Aprili, 2013, Mama Kanisa ameadhimisha Kumbu kumbu ya Siku kuu ya
Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Mtakatifu Yosefu alijinyenyekesha
mbele ya Mungu kiasi hata cha kudiriki kuchukua dhamana ya kuitunza Familia Takatifu
sanjari na kuokoa maisha ya Bikira Maria na Mtoto Yesu yaliyokuwa hatarini, kielelezo
cha unyenyekevu katika kuukubali mpango wa Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi
Mungu ni mwingi wa huruma, upole na mnyenyekevu, fadhila ambayo imejionesha kwa namna
ya ajabu katika maisha ya Yesu Kristo, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, changamoto
kwa Wakristo kujinyenyekesha ili kukua na kukomaa katika misingi ya imani, matumaini
na mapendo.
Lengo ni kutoa fursa kwa mbegu ya upendo wa Mungu kuota na kukomaa
katika hija ya maisha ya mwamini. Fadhila ya unyenyekevu katika upendo inajionesha
kwa namna ya ajabu katika Fumbo la Msalaba: yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Bila unyenyekevu, upendo utashindwa kutua nanga katika moyo na maisha ya mwamini.
Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia fadhila ya unyenyekevu.