Amani na utulivu katika eneo la Maziwa Makuu ni kati ya changamoto kubwa inayozikabili
Tume za Haki na Amani katika nchi za Maziwa Makuu, Ukanda wa Afrika. Hii inatokana
na ukweli kwamba, Ukanda huu mara kadhaa umekuwa ni uwanja wa vita na mauaji ya kimbari,
mambo yanayokwamisha juhudi za kuleta haki, amani, upendo, mshikamano na maendeleo
endelevu.
Kutokana na changamoto hizi, hivi karibuni, Tume ya haki na amani
ya Jimbo Katoliki Kyangugu, ilifanya mkutano na wadau wa haki na amani Jimbo Katoliki
la Bukavu, DRC.
Lengo la mkutano wa tume hizi kadiri ya habari kutoka Baraza
la Maaskofu Katoliki Rwanda ni kujaribu kupunguza hali ya kinzani inayoendelea kujitokeza
baina ya nchi hizi mbili kiasi cha kutishia masuala ya usalama na amani katika eneo
la Maziwa Makuu. Mkutano huu ulisimamiwa na kuongozwa na Askofu mkuu Fracois Xaver
Maroy, wa Jimbo kuu la Bukavu, DRC na Askofu Jean Damascene Bimenyimana wa Jimbo Katoliki
la Kyangugu, Rwanda.
Mkutano huu umehudhuriwa na Maparoko wanaohudumia Parokia
za mpakani kati ya Rwanda na DRC, kwa pamoja walilenga kutafuta na kuendeleza mambo
yanayodumisha misingi ya haki na amani pamoja na kudumisha uhusiano mwema kati ya
wananchi wa nchi hizi mbili.
Hizi zote ni juhudi za kuhakikisha kwamba, waamini
wanatolea ushuhuda wa imani yao katika matendo kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, unaokwenda sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican pamoja na miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipochapisha
kwa mara ya kwanza Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa Kanuni ya Imani,
Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala.
Wajumbe wa mkutano huu
kwa pamoja wameaziamia kwamba, Mapadre, Watawa na Waamini walei wajenge utamaduni
wa kukutana mara kwa mara ili kujadiliana mambo msingi yanayowaunganisha kwa kushirikiana
kwa karibu zaidi ili kuondoa dhana ya uadui na uhasama inayoendelea kujengeka miongoni
mwa wananchi wa pande hizi mbili kiasi cha kutishia misingi ya haki, amani, utulivu
na usalama katika eneo la Maziwa Makuu.
Kwa pamoja, wamedhamiria kuenzi utamaduni
wa haki na amani na kwamba, vita ni mfumo ambao kwa sasa umepitwa na wakati, watu
wanapaswa kujenga utamaduni wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto zao kwa
njia ya majadiliano ya kina yanayoheshimu ukweli, uwazi upendo na mshikamano wa kitaifa,
daima wakitafuta mafao ya wengi.