2013-04-08 09:38:46

Waamini iweni mashahidi na vyombo vya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Huruma ya Mungu, alifunga rasmi kipindi cha Oktava ya Pasaka kwa kusali na waamini pamoja na mahujaji waliokuwa wamemiminika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumiwa na Mama Kanisa katika Kipindi cha Pasaka.

Amani iwe kwenu! anasema Baba Mtakatifu si tu salam na matashi mema kutoka kwa Kristo bali ni zawadi na neema ya Kristo anayowashirikisha mitume wake, baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Anawapatia zawadi ya amani kama alivyokuwa amewaahidia kwani ni matunda ya ushindi wa Mungu dhidi ya ubaya na kielelezo makini cha msamaha. Amani ya kweli inapatikana kwa kufanya mang'amuzi ya ndani juu ya huruma ya Mungu.

Jumapili ya huruma ya Mungu ilianzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili na kadiri ya mapenzi ya Mungu, siku iliyotangulia Jumapili hii, Papa Yohane Paulo wa pili akaaga dunia, yapata miaka minane iliyopita.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Yesu aliwatokea mitume wake mara mbili wakiwa wamejifungia ndani kwenye chumba cha juu. Mara ya kwanza ni siku ile ya Jumapili ya Pasaka, alipofufuka kutoka katika wafu. Siku ile Mtume Tomaso hakuwepo pamoja na mitume wengine, alipoambiwa hakuamini katu katu!

Baada ya siku nane, Yesu aliwatokea tena Mitume wake, akamwalika Toma kuangalia na kugusa madonda yake matakatifu, hapo ndipo Mtume Tomaso alipokiri kwa sauti akisema, "Mungu wangu na Bwana wangu". Yesu akamwambia "wewe kwa kuwa umeniona umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki".

Wale wasioamini wakasadiki, anasema Baba Mtakatifu Francisko ni mitume wengine pamoja na watu waliokuwepo mjini Yerusalem kwa wakati huo, lakini kutokana na ushuhuda wa Mitume waliweza kuamini. Hii ni heri ya Imani, kwa wote wanaomwamini Mungu aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kila wakati na kila mahali kuna watu wenye heri wanaomwamini Kristo kwa njia ya Neno la Mungu linalotangazwa na Kanisa na kushuhudiwa na wa waamini; wale wanaomwamini Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kielelezo cha hali ya juu cha upendo wa Mungu na huruma ya Mungu. Hili ni jambo muhimu kwa kila mwamini.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, Kristo aliwakirimia wafuasi wake zawadi ya amani na Roho Mtakatifu ili waweze kusambaza Msamaha wa Dhambi na Huruma inayotolewa na Mwenyezi Mungu peke yake iliyogharimiwa kwa damu azizi ya Kristo. Mama Kanisa anatumwa na Kristo Mfufuka kuwatangazia watu maondoleo ya dhambi, ili kujenga na kuimarisha ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na upendo. Amani hii ijioneshe katika uhusiano wa kijamii na kwenye taasisi mbali mbali.

Roho wa Kristo mfufuka anafukuza giza na woga kutoka katika mioyo ya wafuasi wake, kutoka ndani walikojifungia kwenye chumba cha juu na kwenda kutangaza Injili. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa na ujasiri wa kuweza kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka; wajitahidi kujitambua kwamba, wao ni Wakristo na kuishi Kikristo. Waamini wawe na ujasiri wa kumtangaza Kristo mfufuka, kwani Yeye ndiye amani yao, aliyewakarimia amani na msamaha kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa mbingu amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili jioni angeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kusimikwa rasmi kama Askofu wa Roma. Anawaalika kutegemea huruma ya Kristo anayeendelea kuwapenda na kuwasubiri ili kuwaonjesha huruma yake, wakati wote wanaokimbilia huruma na msamaha kutoka kwa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru waamini waliosali pamoja na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Roma kwenye Madhabau ya Bikira Maria wa Huruma yaliyoko mjini Roma. Amewataka waamini kwa mara nyingine tena kuwa ni mashahidi na vyombo vya huruma ya Mungu.

Amewataka pia wanachama wa Chama cha kitume cha Wakatukumeni wapya kutekeleza kwa uaminifu utume wao wa kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za maisha, kwa upole na heshima; wawatangazie watu kwamba, Yesu Kristo aliyefufuka ndiye Mkombozi wa dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.