2013-04-08 08:53:02

Simameni kidete kutetea zawadi ya uhai, maadili, utu wema na utunzaji bora wa mazingira


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, limewaandikia waamini Barua ya kichungaji likiwataka kusimama kidete katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu na vikwazo vingi wanavyoendelea kukabiliana navyo katika hija ya maisha yao kama waamini.

Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini ulitanguliwa na semina maalum kuhusu tasaufi ya utumishi pamoja na urithishaji wa imani, kama walivyofafanua Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya.

Maaskofu pia wameangalia utekelezaji wa mikakati ya Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 tangu Ukristo ulipoingia nchini humo, kipindi cha miaka tisa kuanzia sasa. Mkutano huu ulifunguliwa kwa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, yaliyotumwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Askofu mkuu Giuseppe Pinto, Balozi wa Vatican nchini Ufilippini.

Maaskofu wameonesha mshikamano wao wa dhati na wananchi wa Ufilippini walioathirika kutokana na tufani zilizowakumba kwa siku za hivi karibuni, kiasi cha kusababisha maafa makubwa nchini humo. Watu wengi wamepoteza maisha, mali pamoja na miundo mbinu kuharibiwa vibaya. Maaskofu wanasema kwamba, athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoendelea kuleta maafa makubwa nchini humo na sehemu nyingine duniani ni matokeo ya binadamu kutozingatia sheria na kanuni za utunzaji bora wa mazingira.

Kuna ukataji ovyo wa miti pamoja na uchimbaji mbaya wa madini, usiozingatia mafao ya wengi na badala yake, wawekezaji wanajikuta wakielemewa zaidi na faida, kuliko hasara zinazoweza kujitokeza kwa siku za baadaye. Maafa yote haya ni changamoto kwa wananchi na viongozi nchini humo kufanya tafakari ya kina kuhusu ukweli, ubora na tija inayotolewa na viongozi hawa kwa ajili ya mafao ya wengi, kama sehemu ya mchakato wa uwajibikaji na utendaji makini wa shughuli za uongozi.

Licha ya maafa makubwa yaliyosababishwa na tufani hizi, lakini pia wananchi wa Ufilippini wanakabiliwa na maafa makubwa kutokana na baadhi ya viongozi wao wanaokumbatia utamaduni wa kifo kwa kutaka kuiga sera na vipaumbele vya Nchi za Magharibi, ambavyo wakati mwingine vinasigana na maadili na utu wema. Baadhi yao wamejikuta wakizama katika rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali ya umma, kwa kujiundia makundi ya wanasiasa wanaojitafuta badala ya kutafuta mafao ya wengi.

Ni changamoto ya kuwa waaminifu katika kanuni za uongozi, daima wakitafuta Haki Jamii, Mafao ya Wengi pamoja na kukumbatia zawadi ya maisha. Ni jambo lisilokubalika kwamba, kuna watu wanaendelea kupoteza maisha yao, kutekwa na kubakwa, wakati kuna sheria na vyombo ambavyo vinapaswa kusimamia sheria na kanuni za nchi. Kuna haja kwa viongozi wa namna hii kuwajibishwa barabara, ili haki, amani na utulivu viweze kutawala tena miongoni mwa wananchi wa Ufilippini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linasema, msimamo wa Kanisa Katoliki ni kuendelea kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hawakubaliani na sera na sheria za afya ya uzazi zinazotaka kukumbatia utamaduni wa kifo pamoja na kupelekea kumong’onyoka kwa maadili na utu wema nchini humio kwa kizingizio cha kutaka kupata misaada ya kiuchumi.

Maaskofu wanasema, rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ni kati ya majanga makubwa yanayodhalilisha utawala bora na uongozi wa sheria. Ikumbukwe kwamba, viongozi wanapaswa kusimamia mafao ya wengi na nafasi za uongozi walizokabidhiwa na jamii si kwa ajili ya kujitafuta na kwa ajili ya masilahi yao binafsi. Wananchi wawe makini katika kuwaangalia viongozi wa aina hii na wawe na ujasiri wa kuwanyima kura wakati wa uchaguzi mkuu.

Maadili na utu wema, upendeleo kwa maskini ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee ili kuleta maboresho ya maisha ya wananchi wengi wa Ufilippini wanaoogelea katika umaskini wa kipato, kinzani na migogoro ya kijamii. Waamini na wananchi kwa ujumla wajitahidi kufuata dhamiri zao nyofu na kamwe wasikubali kushinikizwa kutenda mambo ambayo yako kinyume cha dhamiri nyofu, utu na maadili mema.

Maaskofu hali wameshikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro wanasema, wataendelea kutangaza ukweli na kutweka hadi kilindini, pasi na woga wala wasi wasi katika maji marefu yanayoonesha kukengeuka kwa binadamu. Kanisa linafanya yote haya likisukumwa na imani, maadili na utu wema, daima likitafuta mafao ya wengi.

Kanisa linaendelea kuhimiza waamini na wananchi katika ujumla wao kufuata njia ya mpango wa uzazi asilia, unaoheshimu zawadi ya maisha na kuwawajibisha wanandoa, kama sehemu ya kuenzi Injili ya Maisha. Vijana wajitahidi kujizuia, kusubiri na kuwa waaminifu katika mahusiano yao, wakitambua kwamba, bado Ukimwi ni janga la Kimataifa.

Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa hatua mbali mbali zilizochukuliwa nchini humo katika kulinda na kudumisha haki, amani na utulivu na kwamba, amani ni matunda ya haki. Kanisa, litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa: maskini, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mwishoni wanasema, wote hawa hawana budi kutangaziwa kweli za Injili zinazogusa undani mwa mtu: kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.