Mama Kanisa tarehe 8 Aprili 2013 anafanya Kumbukumbu ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa
habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Hii ni siku ambayo Mashirika mengi ya kutetea
uhai wa mwanadamu yanaitumia kupinga utamaduni wa kifo unaoendelea kuku ana kupanuka
kwa kasi ya ajabu sehemu mbali mbali za dunia. Siku ya kutetea
uhai ni mwaliko wa Kanisa kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema kuendelea kuenzi
Injili ya Uhai kama alivyobainisha Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake
kichungaji, Injili ya Uhai. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho
ya Siku ya Uhai Kimataifa, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama
kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni
mwa Mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Maaskofu
wanakumbusha kwamba, maisha ya mwanadamu ni matakatifu na zawadi ya pekee kabisa kutoka
kwa Mwenyezi Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ya mwanadamu daima
yanaonesha uhusiano na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumbaji. Kutokana na ukweli huu,
kila tendo linalokwenda kinyume cha uhai wa mwanadamu ni jambo ambalo linapingana
na haki na ukweli na hivyo ni kosa pia dhidi ya Mwenyezi Mungu. Baraza la Maaskofu
Katoliki Hispania linawataka waamini, watunga sheria na sera kuhakikisha kwamba, wanathamini
zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. Hii ni haki
msingi kwa kila mwanadamu, inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Maaskofu
wanakumbusha kwamba, hii si zawadi inayotolewa na Serikali kwa wananchi wake, bali
ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe. Serikali zinawajibu wa kulinda na kutetea
zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo, katika kila hatua yake ya maisha. Kanisa
linapenda kujenga na kuimarisha dhamiri nyofu ili watu watambue haki msingi za binadamu
pamoja na umuhimu wa maadili na utu wema katika sheria na sera zinazotungwa na wanasiasa,
ili ziweze kusimamia mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Vitendo vya utoaji
mimba ni ukatili dhidi ya watoto ambao hawajazaliwa; watoto ambao wana haki zao msingi.
Ni jukumu na dhamana ya Serikali kuhakikisha kwamba, inadumisha utamaduni wa uhai
kwa watu wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linasema, litaendelea kutoa
huduma kwa Familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha; huduma kwa wanawake wajawazito
ili kuwasaidia kupokea na kutunza zawadi ya uhai kadiri ya mpango wa Mungu. Kanisa
litaendelea kuwahudumia pia wanawake wanaokabiliwa na shinikizo la utoaji mimba kutoka
katika Jamii, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, bila kusahau huduma kwa wanawake
waliojifungua. Ili kuweza kufanikisha sera na mikakati hii ya shughuli za kichungaji,
kuna haja ya Kanisa kuwa na Mapadre, Watawa na Waamini walei walioandaliwa barabara
ili kuweza kutekeleza utume huu nyeti kwa ajili ya huduma kwa Injili ya Uhai.