Mwenyeheri wa kwanza kutangazwa katika utume wa Papa Francisko
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu, Jumapili iliyopita amemtangaza Cristoforo wa Mtakatifu Katarina
aliyejulikana kwa wakati huo kama Cristoforo Fernàndez Valladolis aliyeishi kunako
mwaka 1638 hadi mwaka 1690, mwanzilishi wa Shirika la Wahudumu wa Hospitali wa Yesu
wa Nazareti kuwa Mwenyeheri.
Ibada hii imefanyika Jimboni Còrdoba, Hispania,
baada ya kukamilika mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri ulioanza kunako mwaka 1773
na hawamu ya kwanza kuhitimishwa Desemba 2012. kardinali Amato ametekeleza utume huu
kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Huyu anakuwa ni Mwenyeheri wa kwanza kutangazwa
katika utume wa Papa Francisko.
Cristoforo Fernandès akiwa na umri wa miaka
kumi alijiunga na Shirika la Ndugu Wadogo Wafransikani wa Mama Yetu wa Antigua, lakini
hakuruhusiwa kukaa Shirikani humo na hivyo kumrudisha nyumbani kwao ambako Mama yake
alikuwa anamsubiri kwa hofu na mashaka makubwa.
Akiwa nyumbani kwao, aliendelea
na masomo, akakuza tasahufi ya toba na huruma kwa wagonjwa. Katika ujana wake, aliweza
kutambuliwa na wengi kuwa ni mtawa aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wagonjwa
na wote waliokuwa wanateseka.Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na Kipadre,
akapadrishwa kunako tarehe 10 Machi 1663.
Kunako mwaka 1668 akaanza Shirika
kwa ajili ya kuwasaidia wakulima waliokuwa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha,
baada ya tafakari ya kina, akatambua kwamba, Kristo alikuwa anamwalika kujitoa bila
yakujibakiza kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wazee, kiasi cha kuanzisha Shirika
la kuwahudumia watu hawa kunako mwaka 1673.
Ni mtawa aliyeonesha weledi mkubwa
katika masuala ya uongozi, utawala na usimamizi mzuri wa mali ya Kanisa, watu wakaonja
upendo wa Mungu, kiasi kwamba, wakawa tayari kumpatia misaada kwa ajili ya maskini,
kwani walimwamini kutokana na matumizi bora ya fedha walizokuwa wanampatia. Changamoto
na uaminifu kwa mali ya Kanisa inayotolewa kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wagonjwa.
Watu
wengi nchini Hispania wakatambua ndani mwake imani, mapendo, huruma, ukarimu, moyo
na bidii ya kazi, kwa wale wote waliobahatika kukutana na kuhudumiwa naye. Akiwa amechoka
na kudhoofu kutokana na huduma kwa wagonjwa waliokuwa wamekumbwa na magonjwa ya mlipuko
tarehe 24 Julai 1690 afariki dunia na akazikwa ndani ya Hospitali aliyoianzisha kwa
mikono yake mwenyewe. Baadhi ya watawa wa Shirika lake, wanatekeleza utume wao Barani
Ulaya na Afrika.