Waandishi wa habari Majimboni, tafuteni mbinu za kukabiliana na changamoto ya Uinjilishaji
katika maeneo yenu!
Wafanyakazi kutoka katika Idara za Upashanaji habari za majimbo Katoliki DRC, kwa
muda wa siku mbili kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi 6 Aprili 2013 wamepata fursa ya kukutanika
na kujadili kwa pamoja changamoto wanazokabiliana nazo katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya nchini mwao, kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na maendeleo
ya sayansi na teknolojia katika mawasiliano ya Jamii.
Akizungumza katika mkutano
huu, Padre Jean-Marie Bomengola, Katibu wa Idara ya Upashaji Habari, Baraza la Maaskofu
Katoliki DRC, amewataka wadau hawa ambao wana mchango mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji
kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa ukamilifu mkubwa dhamana waliyokabidhiwa na Mama
Kanisa katika Majimbo husika. Wanahabari kutoka Majimboni wanapaswa kujipanga vyema
ili kukabiliana na changamoto za upashanaji habari zinazoendelea kuibuliwa na vyombo
vya habari duniani.
Akizungumza kwa niaba ya Askofu Nicolas Djomo, Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, Padre Felicien Mwanama, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza
la Maaskofu Katoliki DRC amewashukuru wajumbe kwa mchango wao mkubwa katika ulimwengu
wa upashanaji habari.
Amewaalika kutumia mkutano wa wanahabari kutoka Majimboni
kubadilishana uzoefu, ujuzi na mang'amuzi mbali mbali ili waweze kufanya maboresho
makubwa katika idara za mawasiliano ya Jamii kutoka katika majimbo mbali mbali nchini
DRC. Ni mwaliko wa kusoma alama za nyakati na kujibu matarajio ya waamini wanaowahudumia
kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya Jamii.