2013-04-06 10:07:34

Papa Francisko: mwanadamu anapata ukombozi kwa Jina la Yesu Kristo


Mwanadamu anapata wokovu kwa jina la Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu na wala si kwa juhudi zake binafsi au maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, Ijumaa ya Kipindi cha Oktava ya Pasaka katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichopo mjini mjini Vatican na kuhudhuriwa na Watawa wa Shirika la Fatebenefrateli pamoja na wafanyakazi wa Famasia ya Vatican.

Baba Mtakatifu alikuwa anatafakari pamoja nao sehemu ya Matendo ya Mitume: 4: 1-12, kuhusu maana na umuhimu wa Jina la Yesu, baada ya Mitume Petro na Yohane kukamatwa na kupelekwa mbele ya Baraza kuu la Wayahudi, wakishambuliwa kwa kuulizwa ni kwa nguvu gani na kwa jina la nani wameweza kufanya muujiza wa kumponya yule kiwete. Wao bila woga wala wasi wasi wakajibu wakisema ni kwa Jina la Yesu Kristo, Jiwe lile walilokataa waashi sasa limekuwa ni jiwe kuu la pembeni.

Yesu Kristo ndiye Mkombozi wa dunia, ndiye anayeendelea kutenda miujiza miongoni mwa wafuasi wake. Jina la Yesu ambalo limepigwa chapa mioyoni mwa waamini, linaendelea kuwaongoza katika safari ya maisha yao ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, hata muujiza uliofanywa na Mtume Petro na wenzake walipoambiwa kutweka hadi kilindini bila ubishi ni mwendelezo wa maajabu ambayo Yesu anafanya kwa njia ya mitume wake. Kuna uhusiano kati ya Yesu Kristo na Roho Mtakatifu, kwani waamini wanaweza kuungama, kushuhudia na kuzungumza kuhusu Jina la Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu, changamoto kwa waamini kuwa na imani thabiti kwa Yesu Kristo anayeandamana pamoja nao katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Kwa mtu mwenye imani thabiti, anapolitaja Jina la Yesu anakuwa na nguvu ya kuweza kutekeleza majukumu yake barabara, kwani anatambua uwapo na ulinzi wake madhubuti, kama alivyowahi kusimuliwa na Mzee mmoja aliyekuwa amebahatika kupata watoto wanane katika maisha yake. Kwa njia ya neema ya Ubatizo aliyoipokea aliweza kutekeleza wajibu wake kwa kutambua kwamba anaye Yesu anayeandamana naye katika hija ya maisha yake! Ni mwaliko wa kumtazama na kumtumainia Kristo Mkombozi wa dunia badala ya kuwakimbilia "wakombozi uchwara" wanaojitokeza kila kunapokucha!

Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, kwa waamini walio wengi, wanamkimbilia Yesu pale wanapokabiliwa na shida na magumu ya maisha, lakini pale mambo yanapowaendelea sawa; Yesu hana nafasi tena katika maisha yao na matokeo yake wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji na wapiga ramli!

Waamini kwa namna ya pekee wanachangamotishwa na Baba Mtakatifu Francisko kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Jina la Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Anawakumbusha waamini kwamba, Bikira Maria anawasaidia kuwaonesha njia inayomwendea Yesu Kristo, lakini wajifunze kutekeleza yale ambayo wanaambiwa na Yesu, kama ilivyokuwa wakati ule kwenye Harusi ya Kana.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiachilia mikononi mwa Jina la Yesu, ili waweze kupata kitulizo katika maisha yao ya kiroho!







All the contents on this site are copyrighted ©.