Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni alikutana na kuzungumza na Kardinali Angelo
Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu
na kumpatia ruhusu ya kuchapisha hati ya mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri.
Muujiza ambao
umethibitishwa ni kutokana na maombi yaliyotolewa kwa Mtumishi wa Mungu Maria Theresa
Bonzel, mwanzilishi wa Shirika laWatawa wa Mtakatifu Francisko wa Ibada ya Ekaristi,
aliyezaliwa kunako mwaka 1830 na kufariki dunia tarehe 6 Februari 1905. MASHAHIDI
WA IMANI: Mtumishi wa Mungu Manuel Basulto Jimenez, Askofu wa Jimbo la Jean, Hispania
pamoja na wenzake watano waliouwawa kutokana na chuki za kiimani nchini Hispania kati
ya mwaka 1936 hadi mwaka 1937. Mtumishi wa Mungu Jose Maximo Moro Briz na waanzilishi
wenzake wanne, Padre kutoka Jimbo la Avilla, Hispania, aliyeuwawa kikatili kutokana
na chuki za kiimani Hispania kunako mwaka 1936. Mtumishi wa Mungu Vladimir Ghika,
Padre kutoka Jimbo kuu la Bucharest, Romania, aliyezaliwa kunako mwaka 1873 na kuuwawa
kikatiliki kutokana na chuki za kiimani mjini Bucharest tarehe 16 Mei 1954. Mtumishi
wa Mungu Joaquin Jovan Marin na wenzake kumi na wanne kutoka Jimbo la Labourer, Hispania,
Mapadre wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, waliouwawa kikatili kutokana na chuki
za kiimani nchini Hispania kati ya Mwaka 1936 hadi mwaka 1938. Mtumishi wa Mungu
Andres kutoka Palazuelo, Mwanashirika wa Ndugu Wadogo Wakapuchini pamoja na wenzake
thelathini na mmoja, waliouwawa kikatiliki nchini Hispania kutokana na chuki za kiimani
kati ya Mwaka 1936 hadi mwaka 1937. Mtumishi wa Mungu Giuseppe Girotti, Padre wa
Shirika la Wadominikani, aliyezaliwa kunako mwaka 1905 na kuuwawa kikatiliki nchini
Ujerumani kunako mwaka 1945 kutokana na chuki za kiimani. Mtumishi wa Mungu Stefano
Sandor, Mtawa wa Shirika la Wasalesiani wa Mtakatifu Bosko, aliyezaliwa huko Hungaria
kunako mwaka 1914 na kuuwawa kikatili kutokana na chuki za kiimani, huko Hungaria
tarehe 8 Juni 1953. Mtumishi wa Mungu Rolando Rivi, Mseminari wa Jimbo Katoliki
la Reggio Emillia-Guastalla, aliyezaliwa kunako tarehe 7 Januari 1931 na kuuwawa kikatiliki
kutokana na chuki za kiimani nchini Italia hapo tarehe 13 Aprili 1945. Baraza la
Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu limetambua na kuridhia
karama za kishujaa zilizooneshwa na Watumishi wa Mungu wafuatao, ambao nao kwa sasa
wanaingizwa katika mchakato wa kutangazwa kuwa ni Wenyeheri. Hawa ni pamoja na: Mtumishi
wa Mungu Eladio Mozaz Santamera, Padre wa Jimbo na Mwanzilishi wa Shirika la Watawa
wa Yosefina wa Utatu Mtakatifu, aliyezaliwa kunako Mwaka 1837 nchini Hispania na kufariki
dunia huko Plasencia, tarehe 18 Machi 1897. Mtumishi wa Mungu Manuel Aparici Navarro,
Padre wa Jimbo aliyezaliwa kunako mwaka 1902 na kufariki dunia tarehe 28 Agosti 1964. Mtumishi
wa Mungu Moises Lira Serafin, Padre wa Shirika la Roho Mtakatifu na Mwanzilishi wa
Shirika la Wamissionari wa Bikira Maria wa Upendo, aliyezaliwa nchini Mexico kunako
mwaka 1893 na kufariki dunia tarehe 25 Juni 1950. Mtumishi wa Mungu Generoso Msulubiwa,
Padre wa Shirika la Wamissionari wa Mateso ya Kristo, aliyezaliwa nchini Italia kunako
tarehe 6 Novemba 1881 na kufariki dunia mwaka 1969. Wengine katika Orodha hii ni
Mtumishi wa Mungu Olinto Marella, Padre wa Jimbo, kutoka Italia aliyezaliwa kunako
mwaka 1882 na kufariki dunia tarehe 6 Septemba 1969. Mtumishi wa Mungu Antoine
Kowalczyk, Bruda wa Shirika la Bikira Maria aliyezaliwa nchini Poland kunako mwaka
1866 na kufariki dunia huko Edmonton, Canada tarehe 10 Julai 1947. Wa mwisho katika
orodha hii ya Waamini walioonesha karama ya kishujaa ni pamoja na Mtumishi wa Mungu
Silvia Ferreiro da Silva, wanamke mlei, aliyezaliwa huko Ureno kunako mwaka 1882 na
kuitupa mkono dunia kunako tarehe 2 Novemba 1950.