Dhibitini nyanyaso za kijinsia ili Kanisa liweze kuheshimiwa na kuthaminiwa linapotoa
ushuhuda wake kwa walimwengu!
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 5 Aprili 2013 amekutana na kuzungumza kwa kirefu
na Askofu mkuu Gerhard Ludwig Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho
Sadikifu ya Kanisa. Katika mazungumzo haya, Baba Mtakatifu aliweza kujulishwa masuala
mbali mbali yanayohusika na Baraza hili la kipapa.
Kwa namna ya pekee, Baba
Mtakatifu Francisko amelitaka Baraza kuendeleza msimamo wa kushughulikia nyanyaso
za kijinsia ndani ya Kanisa kadiri ya sheria, kanuni na maelekezo ambayo tayari yalikuwa
yamekwishatolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Kanisa halina
budi kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya kulinda na kuwatetea watoto wadogo pamoja na
kuhakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake dhidi ya watuhumiwa.
Jukumu
hili linapaswa kutekelezwa na Maaskofu mahalia pamoja na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
duniani. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kuheshimiwa na kuaminiwa
kwa njia ya ushuhuda na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wahanga wa nyanyaso
za kijinsia wanapaswa kusaidiwa na Kanisa. Amewahakikishia sala zake, wale wote waliokumbwa
na nyanyaso za kijinsia.