2013-04-05 08:14:02

Msiogope, ni mimi Jipeni moyo!


Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pia ni Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Pasaka, aliwataka waamini kuwa na matumaini yanayofumbatwa katika ukweli wa maisha kama sehemu ya mchakato wa kuvuka mtikisiko wa uchumi kimataifa unaoendelea kuleta atahri kubwa kwa maisha ya watu wengi. RealAudioMP3
Ujumbe wa Kikristo unafumbatwa katika matumaini na uhalisia wa maisha na wala si katika hofu na woga usiokuwa na msingi. Mama Kanisa anaendelea kusherehekea Siku kuu ya Pasaka kwa sababu Mwenyezi Mungu amemfufua Yesu Kristo kutoka katika wafu na atafanya hivi pia kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kutambua kwamba, mwanadamu si mkamilifu ana mapungufu yake, mwaliko wa kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na huruma kwa kutambua mwaliko na wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Waamini hawana sababu msingi za kukata tamaa kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu, bali wanatakiwa kujifunga kibwebwe kutumia karama na vipaji vyao kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa kwa kuwa na mwono na mwelekeo chanya na wenye matumaini kwa maisha na utume wa Kanisa pasi na kukata tamaa.
Hii ndiyo changamoto iliyotolewa pia na Askofu mkuu Justin Welby alipokuwa anasimikwa rasmi kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury, hapo tarehe 21 machi 2013. Ujasiri na matumaini haya anasema Askofu mkuu Welby yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kusaidia mchakato wa kuleta maboresho katika maisha ya mwanadamu. Hii ndiyo ndoto ya watu wengi kwa sasa.
Katika kipindi hiki cha Pasaka, waamini wanabahatika kusikia kwa namna ya pekee maneno ya Yesu anayewaambia Mitume wake, Msiogope ni Mimi, Jipeni moyo! Ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi kimataifa na maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na mapambano dhidi ya baa la njaa, ujinga na maradhi, kuna haja kwa waamini kujifunga kibwebwe kupambana na changamoto hizi zote wakiwa na ari na moyo wa Kikristo, bila kuogopa!
Kuna haja ya kuwa makini na kamwe wasidanganyike na mikakati na sera zinazotolewa na wanasiasa kwenye majukwaa kwamba, mkwamo wa uchumi utapita katika kipindi cha miaka michache. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mwanadamu hakupewa kipaumbele cha kwanza katika mikakati, sera na mipango ya uchumi kwa wanasiasa wengi na matokeo yake mamillioni ya watu yanaendelea kuteseka kutokana na athari za mtikisiko wa uchumi kimataifa.
Huu ndio ukweli unaojionesha kwa wananchi wa Cyprus wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na athari kubwa za myumbo wa uchumi kimataifa kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa raia na mali zao. Wakati wa Maadhimisho ya Ijumaa kuu, Askofu mkuu Welby aliwaalika waamini kutafakari kwa kina: mateso na kifo cha Kristo Msalabani ili kwa njia ya Fumbo la Msalaba waweze kupata matumaini mapya.
Jamii ijifunze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi badala ya kugubikwa na uroho wa mali na madaraka kwa kuwabeza wanyonge na wale wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii. Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury mapema mwaka huu alikemea sekta ya uchumi na fedha kwa kuwataka wahusika kutoa huduma kwa Jamii badala ya kutaka kuigandamiza kwa sera zake.








All the contents on this site are copyrighted ©.