2013-04-05 09:07:01

Jimbo Katoliki Bukoba: Askofu Rwoma kusimikwa rasmi hapo tarehe 7 Aprili 2013


Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba na Msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Singida, Jumamosi, tarehe 6 Aprili, 2013 atapokelewa rasmi Jimboni Bukoba na kusimikwa kama Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jumapili tarehe 7 Aprili 2013.

Itakumbukwa kwamba, hapo tarehe 15 Januari 2013 Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alikubali kung'atuka kutoka madarakani kwa Askofu Nestori Timanywa na badala yake akamteua Askofu Rwoma kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba na wakati huo huo kuwa pia Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki Singida.

Askofu Rwoma kunako tarehe 19 Aprili 1999 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Singida na kuwekwa wakfu tarehe 11 Julai 1999, kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki Singida. Tangu wakati huo akiwa Jimboni Singida, aliwaandaa waamini na watu wenye mapenzi mema katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo Jimboni Singida.

Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2015 taswira ya Jimbo la Singida ilikuwa ni kuwa na waamini wengi waliokomaa kiimani, wenye ari ya Kuinjilisha kwa kina na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Dhamira iliyoongoza Maadhimisho ya Maandalizi ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo Jimboni Singida ilikuwa ni kudhihirisha uwepo wa Mungu na kueneza Ufalme wake kwa watu wote Jimboni Singida, kwa kuwaendeleza wanadamu: kiroho na kimwili. Jimbo la Singida likajiwekea mikakati ya kutekeleza katika kipindi cha miaka kumi kwa kujielekeza zaidi katika: ujenzi wa umoja na mshikamano Kijimbo, Kukomaa kiimani, kumwendeleza mwanadamu: kiroho na kimwili, kueneza ufalme wa Mungu kwa kuyatakatifuza malimwengu, wakiongozwa na kauli mbiu "Jubilee Singida, Umoja na Mapendo" Kilele cha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo Singida ilikuwa ni hapo tarehe 17 Agosti 2008.

Jimbo la Singida linaendelea kujivunia sera ya kujitegemea kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Katika hotuba yake ya shukrani kwa wageni mbali mbali, aliwaomba waendelee kulikumbuka Jimbo Katoliki la Singida katika ujenzi wa imani ya kweli, umoja, upendo na mshikamano wa Kikristo.

Anatambua changamoto zilizokuwa mbele ya Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki Singida katika mchakato wa kuendelea kukua na kukomaa katika matendo ya imani, upatanisho kwa njia ya haki, amani, umoja na upendo wa dhati.

Askofu Desiderius Rwoma aliwaambia Wakristo kwamba, wamedhamiria kupanda ngazi ya kuelekea katika utakatifu wa maisha kwa njia ya ukomavu wa imani hadi mbinguni. Kwa njia ya Maombezi ya Bikira Maria kwa kutambua kwamba, siri ya kufikia mafanikio haya ni kumwilisha imani katika matendo.

Imeandaliwa na Pd. Richard Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.