2013-04-05 10:47:08

Hija ya imani kuelekea Maadhimisho ya Siku ya 8 ya Familia Kimataifa, huko Philadelphia 2015


Kengele ya uhuru ni alama muhimu sana kwa Jiji la Philadelphia, Marekani, ambalo litakuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa, itakayofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 27 Septemba 2015. Hii ni kengele iliyopigwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1779 kuwaalika wananchi wa Marekani kukusanyika pamoja ili kusomewa tamko la uhuru wa Marekani.

Nembo ya Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa inaonesha kengele ambayo iko kati kati na kuzungukwa na nyota, ili kuonesha umuhimu wa Jiji la Pennsylvania lililosimama kidete kulinda na kutetea haki za kijamii na uhuru wa kidini. Kwa upande wa Kanisa, kengele inagongwa ili kutangaza Habari Njema ya Familia kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoalikwa kwa namna ya pekee, kushiriki katika maadhimisho ya Familia Kimataifa yatakayofanyika nchini Marekani kwa Mwaka 2015.

Katikati ya Nembo kuna Msalaba unaomwonesha Kristo kuwa ni kiini cha Maadhimisho na maisha ya waamini. Inawaonesha watu watano wenye maumbo na umri tofauti; kielelezo cha dhamana zinazotekelezwa na wanafamilia katika hali ya umoja na mshikamano: hawa ni wazazi, watoto, ndugu na jamaa. Baraza la Kipapa la Familia limetumia fursa hii pia kuzindua tovuti itakayokuwa na mambo mbali mbali kuhusiana na Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa kwa Mwaka 2015, itakayofanyika Jijini Philadelphia.

Unaweza kupata habari zaidi kwa kutumia anuani ifuatayo:

www.worldmeeting2015.org

Askofu mkuu Charles Chaput wa Jimbo kuu la Philadelphia ambaye atakuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho haya anasema, Jimbo lake, utakuwa ni mji wa kwanza kabisa nchini Marekani kuweza kuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kunako mwaka 1994.

Lengo ni kuimarisha tunu msingi na maisha ya kifamilia. tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kutafakari tunu msingi za maisha ya kifamilia, fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Viongozi wa serikali kutoka Pennsylvania tangu wakati huu, wanazikaribisha kwa mikono miwili, familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia Jijini humo. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Maadhimisho ya Nane ya Familia Kimataifa, litakuwa ni tukio kubwa linalotarajiwa kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya waamini na wananchi kwa ujumla wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.