Amani si bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa dukani, bali ni zawadi kubwa kutoka
kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko
katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae,
Alhamisi, tarehe 4 Aprili 2013.
Anasema, wafuasi wa Yesu waliokuwa wanakwenda
Emmaus walishangazwa na muujiza wa Yesu alipoumega mkate na hatimaye akatoweka mbele
yao. Baba Mtakatifu alikuwa anafanya tafakari ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu
Luka: 24: 35 - 48.
Mitume wa Yesu walipigwa na bumbuwazi walipomwona na kumsikia
Yesu akizungumza na kula pamoja nao! walijazwa na furaha ya ajabu, kiasi cha kudhani
kwamba wamepagawa anasema Baba Mtakatifu Francisko! Hii ni furaha inayopata chimbuko
lake pale mwamini anapokutana na Yesu katika hija ya maisha yake, tukio ambalo linaacha
alama ya kudumu katika moyo na maisha ya mwanadamu.
Hali hii inapaswa kuleta
faraja kwa waamini hata kama wanakabiliana na hali ngumu katika maisha yao, kwani
hii ndiyo ile amani ya ndani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na uwapo endelevu
wa Yesu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini kuwa na ujasiri
wa kuomba neema hii katika maisha yao; yaani neema ya kukutana na Yesu katika hija
ya maisha yao. Ni mwaliko kwa waamini kudumisha amani na utulivu wa ndani, kwa kumtafakari
Kristo ambaye aliteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kamwe hakupoteza amani,
zawadi ambayo anapenda kuwashirikisha wafuasi wake.
Ibada hii ya Misa Takatifu
imehudhuriwa na wafanyakazi kadhaa wa Vatican. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri
yake kwa kuwataka waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuomba kupata: neema, faraja
na kitulizo kwa kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao. Misa zinazoendeshwa na
Baba Mtakatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae ni nafasi kwake kuweza kukutana,
kuzungumza na hatimaye kufahamiana na wafanyakazi wa Vatican.