2013-04-04 08:12:08

Vijana na changamoto za Maadhimisho ya Mwaka wa Imani!


Karibu sana ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika hema la vijana. Kama unavyofahamu kuwa mwaka huu ni mwaka wa imani. Swali ambalo limekuwa lakujiuliza kwa vijana wengi ni umuhimu wa mwaka huu katika maisha yetu vijana na ni nini tunapaswa kufanya. Hapa ndipo pale ambapo "upele huwa unafika kwa mkunaji". RealAudioMP3
Tafakari yetu itatuchukua majuma machache na tutazingatia zaidi barua ya kitume ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Porta Fidei, Mlango wa Imani.
Mnamo tarehe 11 Oktoba 2012 tulianza rasmi kuadhimisha mwaka wa imani kadiri ulivyotangazwa na kuzindiliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Hilo linakwenda sambamba kabisa na maadhimisho ya miaka hamsini tangu kufunguliwa kwa Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Tarehe hiyohiyo ni kumbukumbu ya miaka ishirini tangu Baba Mtakatifu Mwenye Heri Yohane Paulo wa Pili kuchapisha rasmi Katekisimu ya Kanisa katoliki. Mwaka jana 2012, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kaitisha pia Mkutano Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji mpya. Kilele cha maadhimisho ya Mwaka wa Imani kitakuwa ni hapo tarehe 24 Novemba 2013.
Matukio yote haya yana maana kubwa na umuhimu sana katika maisha yetu vijana. Wapo baadhi ya vijana ambao bado kabisa hawajasikia habari njema ya wokovu kupitia Kristo Yesu, wapo ambao wamesikia lakini hawamwamini mwokozi huyu wa ulimwengu, na wapo vijana wengi tu ambao walimwamini na kumkiri lakini sasa wanamkana kwa maneno na matendo.
Vijana wengine wanajiona kana kwamba wao bado wamo sana ndani ya mstari, lakini katika hali halisi ya maisha imani yao ni ya juu juu sana. Inawezekana nawe ukawa hivyo, imani ambayo haijakomaa au hauishi jinsi inavyopaswa kwa dhati. Tafakari na kisha chukua hatua!
Jaribu kutulia vizuri baada ya kipindi hiki, jiulize wewe binafsi; Je, imani yako kwa Mwenyezi Mungu ni thabiti kiasi gani. Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja. Mwenyezi amekuumba kwa upendo, amekukomboa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, anakuongoza na kukulinda hata sasa, Je, Unaamini kiasi gani yote hayo. Unafahamu ya kuwa wewe ni dhaifu kufuatia dhambi ya asili, Mungu kajifunua kwetu ili tumfahamu vema na tuwe na mahusiano naye mazuri ili siku moja tuishi naye milele.
Je, unafahamu kuwa katuachia Sakramenti saba ishara wazi za neema isiyoonekana, na ya kuwa Ubatizo ni mlango wa Imani. Je wafahamu na kuamini kwa dhati ya kuwa Kristo yupo katika Ekaristi Takatifu, ya kwamba ni Yeye haswaaa katika maumbo ya mkate na divai. Je, wafahamu na kuamini kuwa mateso na mahangaiko ya leo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na kuwa yana pata maana mpya kupitia mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Je, unaamini kwa dhati ya kuwa kifo si mwisho, sio nukta bali ni njia ya kuonana na kuishi na Mwenyezi Mungu milele. Je una imani thabiti juu ya walio tutangulia mbinguni, juu ya Malaika, juu ya ufufuko wa wafu, juu ya uzima wa milele.
Mpendwa kijana, haya ni maswali msingi yanayohusu imani yetu. Yapo maswali mengine mengi ambayo ningependa kutafakari pamoja nawe leo. Lengo si kutaja yote bali kukupa mwanga tu juu ya uthabiti wa imani yako. ni wakati wakujitazama na kujitafakari kwa kina juu ya kile unachoamini, jinsi unavyoamini na kutoa ushuhuda wa kweli, kwa uhuru na fahari zote juu ya imani yako kwa Mwenyezi Mungu kadiri ya mafundisho ya Kristo na Kanisa lake.
Mababa wa Mtaguso wa pili wa Vatikano waliweka bayana namna yetu ya kuamini katika nyakati hizi. Mwenye Heri Yohane Paulo wa Pili ametuandalia muhtasari wa mafundisho na imani yetu.
Baba Mtakatifu Paulo wa sita aliitisha mwaka wa imani mnamo 1967 na sasa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ameitisha tena mwaka wa imani 2012/13. Hizi ni fursa kwa hakika kwako kijana kuingia kwa undani zaidi katika kuamini na kuishuhudia imani yako bila kujali kejeli, kubezwa, starehe, mitindo ya kisasa na kadhalika.
Chukua fursa hii kutoa ushuhuda wa kweli wa imani yako kwa Kristo. usionee aibu msalaba wa Kristo bali ujisikie fahari na kuukumbatia katika maisha yako ya kila siku ukitambua kuwa furaha ya ufufuko ipo nawe siku hadi siku.
Mimi ntakuwa nawe kwa muda katika kutafakari kwa pamoja mwaka huu wa imani na umuhimu wake katika maisha yako kijana. Usicheze mbali na kipindi hiki cha vijana kila juma, wakati na siku kama leo. Angalia usijekosa uhondo kwani hujui kila juma ntakuwa natokelezea kwa namna gani. Nimekukusanyia vipisi vya maana, naviachalia kwa utaaratibu. Kazi kwako kutumia.
Basi muda ndio hivyo tena, tuonane juma lijalo tena. Toka Studio za Radio vatikani, ni sauti ya kinabii, Padre Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.