Umoja wa Mataifa katika harakati za kudhibiti biashara ya silaha kimataifa
Hatimaye, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amefurahishwa na ujasiri
uliooneshwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kuridhia Mkataba wa Udhibiti
wa Biashara ya Silaha Kimataifa kwa kusema kwamba, huu ni ushindi wa Jumuiya ya Kimataifa.
Mkataba huu utakuwa ni msaada mkubwa wa jitihada za Jumuiya ya Kimataifa katika kudhibiti
vitendo vya jinai, mashambulizi ya kigaidi na chokochoko zinazoendeshwa na mababe
wa vita sehemu mbali mbali za dunia.
Ni mkakati madhubuti unaopania pamoja
na mambo mengine kulinda na kutetea haki msingi za binadamu hatua kubwa katika jitihada
za Jumuiya ya Kimataifa za kupiga rufuku silaha za mahangamizi ambazo zimekuwa ni
tishio kwa binadamu. Hizi ni juhudi na kampeni iliyofanywa usiku na mchana na vyama
vya kiraia, anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Baraza kuu la Umoja wa
Mataifa limepitisha Mkataba wa Kudhibiti Biashara ya Silaha Kimataifa kwa kuungwa
mkono na nchi wanachama 154; Syria, Korea ya Kaskazini na Iran zilipinga muswada huu
na nchi nyingine 23 hazikupinga wala kuukataa Muswada wa Mkataba huo ambao umepata
baraka kubwa kutoka kwa Rais Barack Obama wa Marekani katika mchakato wa kudhibiti
silaha nchini Marekani. Wachunguzi wa mambo wanasema, huu ni mkataba wenye nguvu,
wenye uwiano mzuri na unaotekelezeka.
Mwanzoni, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
alionesha masikitiko yake pale ambapo Mkataba huu ulipoanza kupingwa na Iran, Korea
ya Kaskazini na Syria. Mkataba huu ambao unapongezwa na nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa, kwa mara ya kwanza unaweka vigezo vya kimataifa kwa ajili ya biashara ya
silaha kimataifa; kwa kuzingatia haki msingi za binadamu pamoja na udhibiti wa silaha
ndani ya nchi.
Wafanyabiashara wa silaha kimataifa watapaswa kuzingatia na
kuheshimu vikwazo vya silaha vilivyowekwa kwa baadhi ya nchi; pale ambapo kuna vitisho
vya mauaji ya kimbari pamoja na vita. Ni jukumu la kila nchi kupima na kuangalia ikiwa
kama silaha zilizoko nchini mwake zinatumika katika masuala ya uvunjaji wa haki msingi
za binadamu, vitendo vya kigaidi au makosa ya jinai.