2013-04-04 09:56:43

Siku ya Kimataifa dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 4 Aprili 2013 inaadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini, jitihada zilizoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa kunako mwaka 1997. Bado kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuhamasisha utokomezaji wa mabomu ya kutegwa ardhini kama sehemu ya mchakato unaopania kulinda na kudumisha maisha; misingi ya amani na maendeleo hasa katika nchi zinazoendelea.

Umoja wa Mataifa bado unaendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa mamillioni ya watu walioathirika kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini huko Afghanistan, Cambodia, Colombia, Laos, Lebanon, Sudan ya Kusini na sehemu mbali mbali duniani. Kuna haja ya kuongeza kasi ya kutegua mabamu haya kutokana na ukweli kwamba, mgogoro wa kivita nchini Syria na Mali unatishia usalama wa maisha ya watu.

Hayo yamo kwenye Ujumbe wa Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini. Jumla ya nchi 161 za Umoja wa Mataifa zimetia sahihi kwenye itifaki hii ambayo ilipitishwa kunako mwaka 1997. Hadi sasa ni nchi 127 ambazo zimeridhia Mkataba huu kuhusu haki msingi za watu wenye ulemavu. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayaomba mataifa wanachama kuridhia itifaki hii ili iweze kutumika kwa nchi zote za Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa katika mikakati yake unaendelea kutoa fursa kwa shughuli za uokoaji, uimarishaji wa amani, maendeleo pamoja na kuwasaidia waathirika wa mabomu haya; wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Mikakati ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2013 hadi mwaka 2018 unapania kujenga na kuimarisha mazingira ya usalama ili kutoa fursa ya kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika maisha ya kiuchumi na kijamii na waathirika waweze kupewa haki zao msingi na kutambuliwa kuwa ni sehemu ya Jamii husika.







All the contents on this site are copyrighted ©.