2013-04-04 08:24:03

Changamoto za Uinjilishaji Mpya mintarafu mchango wa Kardinali Jorge Mario Bergoglio


Kardinali Jaime Lucas Ortega Alamino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Havana, Cuba, akishirikisha mang’amuzi yake kutokana na mikutano elekezi iliyofanywa na Makardinali wakati wa mchakato wa kumchagua Papa Mpya anabainisha kwamba, tafakari iliyotolewa na Kardinali Jorge Mario Bergoglio ilikuwa wazi na dira muhimu sana kwa Mama Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto inayovaliwa njuga wakati huu. RealAudioMP3
Anasema, alishiriki kikamilifu katika kumuaga Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyeng’atuka kutoka katika uongozi ili kupata muda zaidi wa kusali na kutafakari kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la Kristo. Kardinali Bergoglio alitoa changamoto ya kina kuhusu maisha na utume wa Kanisa mintarafu changamoto za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Kardinali Ortega anasema, aliposikiliza tafakari hii, alikwenda moja kwa moja kwa Kardinali Bergoglio ili kuomba karatasi ya tafakari yake naye bila uchoyo wala roho ya kwanini, akampatia kikaratasi kilichokuwa kimeandikwa kwa mkono, kuonesha mawazo yake makuu katika mkutano elekezi kwa Makardinali wakati wa mchakato wa kumchagua Papa Mpya.
Kardinali Bergoglio alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa mara nyingine tena Kardinali Ortega alimwomba ruhusa ya kutumia mawazo yake kwa ajili ya kuwashirikisha waamini wake wakati huu Kanisa linapoendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya.
Kardinali Bergoglio katika hotuba yake kwenye mkutano wa Makardinali, alikazia mambo makuu manne: Uinjilishaji; Kanisa kujikosoa; Kanisa kutoka ndani mwake ili kwenda kuinjilisha pamoja na kumruhusu Kristo kutoka ndani mwao ili kuwaendea wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Kuhusu mchakato wa Uinjilishaji Mpya, Kardinali Bergoglio wakati huo aliwachangamotisha Makardinali kwa kuwaambia kwamba, Kanisa halina budi kutoka ndani mwake, ili kuwaendelea wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii, waliokata tama ya maisha; wanaokabiliana na hali ngumu kutokana uwepo wa dhambi, ukosefu wa haki msingi za binadamu, magonjwa, njaa na ujinga.
Kanisa halina budi kujitoa kimasomaso kwa ajili ya Uinjilishaji badala ya kujitafuta lenyewe, kiasi cha kulitenga na kile kinachoendelea ulimwenguni. Ni mwaliko wa kwenda ulimwenguni ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha amini na adili. Kwa njia hii, Kanisa linaweza kumruhusu Kristo kutoka ndani mwao na kuwagusa wale wanaohitaji kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka.
Kanisa linalojiinjilisha, linapaswa kuwa ni mwanga na chumvi ya dunia, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa ndani ya Kanisa. Mwishoni, Kardinali Bergoglio aliwaasa Makardinali wenzake wawe ni watu wa sala na tafakari ya kina kuhusu Kristo, ili hatimaye, aweze kuwasaidia katika kutekeleza utume wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.
Anasema, kwa namna ya pekee, Kanisa linatumwa kuwaendelea wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii: kiroho na kimwili. Hii ni changamoto kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa linawahitaji watu wanaosali na kufanya tafakari ya kina kuhusu Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka. Viongozi, wawe waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hii ndiyo ile furaha ya Uinjilishaji Mpya!








All the contents on this site are copyrighted ©.