2013-04-04 09:11:37

Baraza la Makanisa Ulimwenguni lapongeza Mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha kimataifa!


Dr. Olav Fyskse Tveit Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amepongeza hatua iliyofikiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha kimataifa. Watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaanza kuwa na matumaini kuhusu usalama wa maisha na mali zao. Mkataba wa udhibiti wa biashara ya silaha kimataifa umeungwa mkono na nchi wanachama 155 hapo tarehe 2 Arpili 2013 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Makanisa Ulimwenguni yamekuwa yakiathirika pamoja na kuendelea kushikamana na waathirika wa vita, migogoro na kinzani za kijamii; mambo ambayo kimsingi ni kikwazo kikuu cha ustawi na maendeleo ya mwanadamu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawashukuru na kuwapongeza wajumbe walioamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa masilahi ya usalama wa binadamu badala ya kutafuta faida kubwa kwa gharama ya maisha ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Makanisa kwa miaka mingi yamekuwa pia mstari wa mbele kupinga biashara ya silaha kimataifa.

Ni wajibu wa viongozi wa Serikali kuhakikisha kwamba, mkataba huu unatekelezeka kwa ajili ya mafao ya wengi. Makanisa yataendelea kuombea misingi ya haki, amani na upatanisho katika nchi ambazo mtutu wa bunduki bado unaendelea kurindima na hivyo kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia. Hali bado ni mbaya huko Syria, DRC, Sudan na Colombia. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa badala ya silaha hizi kuwa ni sababu ya maangamizi, sasa mtaji huu ugeuzwe ili kuleta mafao zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.