Watawa waliotekwa nyara DRC Oktoba 2012 bado hawajaachiliwa
Baraza la Maaskofu Katoliki DRC kwa mara nyingine tena, limetoa wito kwa watu waliowatekwa
nyara watawa watatu wa Shirika la Wasumption wa Mtakatifu Augostino tarehe 19 Oktoba
2012 kuwaachilia ili waweze kuendelea na maisha na utume wa kumtumikia Mungu na jirani
zao.
Watawa walitekwa nyara kutoka katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Maskini,
Jimbo Katoliki la Butembo-Beni na ambao hadi sasa hawajulikani mahali waliko. Hawa
ni: Jean Pierre Ndulani, Anselme Wasinkundi na Edmund Bamutute. Maaskofu wanawaomba
wateka nyara kuwaachilia mara moja watawa hao. Jitihada za kuwatafuta hadi sasa zinaonekana
kugonga mwamba.
Maaskofu mara kadhaa wamewaomba wateka nyara kuwaachilia huru,
kama walivyofanya pia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyofanyika
mjini Vatican, mwezi Oktoba 2012 bila mafanikio. Maaskofu wanasema, bado hawajakata
tamaa wanatumaini kwamba, watawa hawa wataweza kuachiliwa huru na hatimaye, kuendelea
na utume wao!