Uvuvio na ukweli ni mada inayopembuliwa wakati wa Mkutano mkuu wa Mwaka wa Tume ya
Kipapa ya Biblia
Tume ya Kipapa ya Biblia itakuwa na mkutano wake mkuu wa mwaka kuanzia tarehe 8 hadi
12 Aprili 2013 utakaofanyika kwenye Domus Sanctae Marthae chini ya uongozi wa Kardinali
Gerhard Ludwig Muller, Rais wa Tume na Padre Klemens Stock, Katibu mkuu ambaye atasimamia
kazi za mkutano mkuu.
Katika mkutano huu, wajumbe wanatarajiwa kukamilisha
tafakari kuhusu "Uvuvio na Ukweli wa Biblia". Kwa miaka kadhaa, wajumbe wa Tume hii
ya Kipapa wameelekeza nguvu zao zaidi ili kufanya upembuzi yakinifu ili kutambua ni
kwa kiasi gani uvuvio na ukweli unajionesha katika vitabu mbali mbali vya Maandiko
Matakatifu.
Lengo la tafakari hii ya kina ni kutaka kutoa mchango chanya ili
kuwa na uelewa mpana zaidi juu ya maudhui ya uvuvio na ukweli, ili Neno la Mungu liweze
kupokelewa na waamini wote kwa kutambua zawadi hii kubwa ambayo kwa njia yake, Mwenyezi
Mungu anawasiliana na watu na kuwaalika kujenga umoja pamoja naye!