2013-04-03 08:48:16

Umuhimu wa hija za maisha ya kiroho katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, muhtsari wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa, waamini nchini Nigeria wanaalikwa kwa namna ya pekee kushiriki katika hija za maisha ya kiroho zilizopangwa na Parokia, Majimbo na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria.
Hija hizi zinaendelea kufanyika mjini Roma ambako kuna utajiri mkubwa wa ushuhuda wa imani na katika Nchi Takatifu, mahali ambako Yesu alitekeleza utume wake wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Ili waamini waweze kujipatia rehema kamili zinazotolewa na Mama Kanisa katika hija za maisha ya kiroho, wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kutimiza masharti yote yanayotolewa na Kanisa pamoja na kujiandaa vyema katika maisha ya kiroho.

Waamini wanahamasishwa zaidi kwa kufanya toba na kushiriki kwa ufahamu zaidi wa Mafumbo ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limepanga hija tatu za maisha ya kiroho katika maeneo matakatifu. Kati ya hija hizi, moja ni maalum kabisa kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Hija ya kwanza ni ile ambayo imepangwa kwa ajili ya Juma kuu na ilianza tarehe 25 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2013. Waamini watapata fursa ya kutembelea San Giovani Rotondo, Lanciano na Roma. Waamini, wakaadhimisha Fumbo la Pasaka na Papa Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni bahati iliyowangukia wale ambao wameshiriki katika kundi la kwanza katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Kundi la Pili litaanza hija yake tarehe 8 hadi 19 Mei 2013. Hawa watatembelea Israeli, Roma, Cascia na Assisi. Lengo ni kuwawezesha Waamini kuadhimisha Siku kuu ya Pentekoste pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakiwa imara katika imani, matumaini na mapendo, waweze kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, katika maisha na vipaumbele vyao.
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, Kundi la tatu la mahujaji kutoka nchini humo litaanza hija yake tarehe 25 hadi 30 Septemba 2013. Hii ni nafasi ya pekee kwa Makatekista ambao ni wadau wakuu wa Uinjilishaji Barani Afrika kupata nafasi ya kukutana na Katekista Mkuu, Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Maaskofu wanawaomba waamini katika Parokia na Majimbo yao kuwawezesha Makatekista kwa hali na mali ili kushiriki katika hija hii ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Huu ni wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa Makatekista kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaokusanyika hapa mjini Roma kwa wakati huo.
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha kwamba, hija nyingine mbili zilizopangwa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani zitafanywa mjini Roma, Lourdes, Ufaransa na Fatima, Ureno. Kwa waamini watakaokwenda Fatima, watashiriki pia kumbu kumbu ya miaka 96 tangu Bikira Maria wa Fatima alipowatokea wale watoto watatu wa Fatima, yaani Francis, Yacinta na Lucia.

Hija hii itafanyika kuanzia tarehe 8 hadi 9 Oktoba 2013, ili kuwawezesha waamini kushiriki pia katika Sherehe za Kuufunga Mwaka wa Imani, changamoto na mwaliko kwa waamini kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, si tu kwa maneno, bali kwa njia ya matendo yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.