Papa Francisko atembelea na kusali kwenye kaburi la Mwenyeheri Yohane Paulo II
Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka minane tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa
Pili alipofariki dunia, hapo tarehe 2 Aprili 2005, Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne
jioni, alikwenda kutembelea na kusali kwenye kaburi la Mwenyeheri Yohane Paulo wa
pili lililoko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Sebastiani, ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican. Katika ziara hii fupi, Baba Mtakatifu ameandamana na Kardinali
Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja na Monsinyo
Alfred Xuereb, katibu binafsi wa Papa Francisko.
Baba Mtakatifu alitumia fursa
hii kwa ajili ya kusali kitambo na baadaye alitembelea na kusali kwenye makaburi ya
Mwenyeheri Yohane wa Ishirini na tatu na Baba Mtakatifu Pio wa kumi. Hija hizi kwenye
makaburi ya watangulizi wake zinalenga kwa namna ya pekee kuonesha mwendelezo wa maisha
ya kiroho katika kumtukimia Kristo na Kanisa lake.
Ni mwelekeo huu pia ambao
unajionesha kwenye uhusiano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Papa mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, wanapozungumza kwa faragha kwa njia ya simu.