Imarisheni imani yenu kwa Kristo Mfufuka na Kanisa lake ili muweze kuwa ni alama wazi
ya ukuu wa maisha na matumaini dhidi ya ubaya, dhambi na kifo
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 3 Aprili 2013 aliendeleza Katekesi kuhusu
Mwaka wa Imani, zilizokuwa zinatolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita kuhusu: Kanuni ya Imani: Siku ya Tatu Akafufuka kutoka katika wafu kadiri
ya Maandiko Matakatifu.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Ufufuko wa Kristo ni
kiini cha imani ya Kanisa, msingi wa matumaini ya utekelezaji wa ahadi za Mungu pamoja
na ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Mashahidi wa kwanza wa ufufuko wa Kristo walikuwa
ni wanawake; waliosukumwa na upendo kwa Kristo kiasi kwamba, wakajihimu kwenda kaburini,
huko wakapewa Habari Njema ya Ufufuko waliyowashirikisha Mitume.
Baba Mtakatifu
anasema, hii ni changamoto kwa waamini kuweza kushirikisha ile furaha inayopata chimbuko
lake kutoka kwa Kristo Mfufuka. Katika historia ya maisha na utume wa Kanisa, wanawake
wamekuwa wepesi kuwafungulia wengine mlango wa imani kwa Kristo, kwani imani ni jibu
makini la upendo.
Kwa njia ya jicho la imani, waamini pia wanayo bahati ya
kukutana na Yesu Kristo Mfufuka na kuonja uwapo wake: katika Maandiko Matakatifu,
Ekaristi Takatifu na Sakramenti mbali mbali za Kanisa; matendo ya huruma, wema na
msamaha ni matukio ambayo yanaonesha uwapo endelevu wa Kristo katika hija ya maisha
ya wafuasi wake hapa duniani.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Katekesi
yake kwa kuwataka waamini, mahujaji na watu wenye mapenzi mema kuimarisha imani yao
kwa Kristo Mfufuka ili waweze kuwa kweli ni alama wazi ya ukuu wa maisha na matumaini
dhidi ya ubaya, dhambi na kifo.
Akizungumza na waamini na mahujaji katika lugha
mbali mbali, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, amewashukuru Vijana kutoka
Lebanon walioshiriki katika kutunga na kuandika Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka
Magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu jioni.
Anawataka waamini kuongozwa na Mwanga
wa Kristo Mfufuka, ili aweze kuwakirimia nguvu itakayowaletea mabadiliko ya ndani,
ili waweze kuwa ni alama ya maisha yake duniani. Amewatakia wote amani ya Kristo mfufuka
na kuwataka waguswe kwa namna ya pekee na upendo wa Kristo, ili kuutolea ushuhuda
katika maisha adili.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua kwamba, Kanisa
limezaliwa kutoka katika tumbo la Pasaka, mwaliko na changamoto kwa waamini kumtolea
ushuhuda Yesu Kristo Mfufuka; kwa njia ya kuguswa na mahangaiko ya jirani, msamaha,
upendo na huruma kwa wote. Furaha ya Kristo Mfufuka iwashukie na kukaa na familia
zao.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru Kardinali Angelo
Scola wa Jimbo kuu la Milani pamoja na mahujaji 10,000 kutoka Jimboni humo waliofika
mjini Vatican kufanya hija, kama sehemu ya maandalizi ya kupokea Sakramenti za Kanisa
kwa Vijana. Anasali na kuwaombea ili imani yao iweze kukua na kuongezeka na hatimaye,
kuzaa matunda yanayokusudiwa. Anawataka vijana hawa kuongozwa na Injili ya Kristo,
kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi.
Ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari
na kuliishi katika hali ya unyenyekevu na ukawaida; katika hali ya udugu, huduma na
matumaini mbele ya Mwenyezi Mungu na katika furaha ya kuwa na Baba ambaye yuko mbinguni
anayewasikiliza na kuzungumza nao katika mioyo yao. Anawataka vijana kufuata dhamiri
nyofu!