Ujumbe kwa Maadhimisho ya Siku ya 6 ya Ugonjwa wa Mtindio wa Ubongo Kimataifa
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la Wahudumu wa Sekta ya Afya,
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha moyo wa upendo na mshikamano
kwa watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa mtindio wa ubongo pamoja na familia zao, Jumuiya
ya Kimatifa inapoadhimisha Siku ya sita ya Wagonjwa wenye mtindio wa ubongo duniani,
tarehe 2 Aprili 2013.
Askofu mkuu Zimowski anabainisha kwamba, ugonjwa wa mtindio
wa ubongo, licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba, bado wagonjwa
wanaendelea kuangaliwa kwa woga na unyanyapaa. Lakini ikumbukwe kwamba, wote hawa
wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Tangu mwanzo, Kanisa limeonesha upendo na mshikamano
wa pekee kwa watoto wenye mtindio wa ubongo kwa kuwapatia tiba na huduma msingi katika
maisha yao.
Ni mwaliko wa kuendeleza upendo na mshikamano huu kwa wagonjwa
na familia zao kwani hawa ni watu wanaotamani kuthaminiwa, kuonjeshwa furaha na matumaini;
kupendwa na kuhudumiwa kikamilifu; kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa,
kwa kutambua kwamba, hata wao wanapaswa kuonjeshwa zawadi ya imani.
Kwa maneno
machache, Askofu mkuu Zimowski anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa
kweli ni Wasamaria wema, wakijitahidi kumwiga Kristo, kielelezo makini cha Msamaria
mwema, kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake ameweza kuukomboa ulimwengu.
Kanisa
linapofanya kumbu kumbu ya miaka minane, tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Yohane
Paulo wa Pili, hapo tarehe 2 Aprili 2005, Kanisa linawaweka wagonjwa wote wa mtindio
wa akili chini ya maombezi ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, aliyekezia kwamba,
ubora wa maisha ya Jamii yoyote ile unapimwa kwa jinsi gani Jamii inajitosa kimaso
maso kuwahudumia wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kwa kuheshimu
na kuthamini utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Haki
zao zinapaswa kuheshimiwa na kwamba, licha ya ulemavu wanaokabiliana nao, wanapaswa
pia kushirikishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kuwapatia fursa ya kuchangia vipaji
walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii anasema Mwenyeheri Yohane Paulo wa
pili, Jamii itakuwa inatembea katika sheria na haki.
Baba Mtakatifu Francisko
anaendelea kuwaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, waamini
wanashirikiana kuzima kiu ya undani wa maisha yao, kwa kuwa na mwono sahihi wa binadamu
badala ya mwanadamu kugeuka na kuwa kama bidhaa, jambo ambalo ni hatari kwa nyakati
hizi.
Ni matumaini ya Askofu mkuu Zygmunt Zimowski kwamba, waamini na watu
wenye mapenzi mema wataungana kwa pamoja ili kuwaonjesha upendo na mshikamano watoto
wanaokabiliwa na ugonjwa wa mtindio wa ubongo.